IQNA

Jinai za Israel

Ayatullah Sistani akosoa jamii ya kimataifa kwa kushindwa kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni

14:14 - November 05, 2024
Habari ID: 3479703
IQNA-Marja' wa ngazi ya juu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq ameeleza masikitiko yake kuhusu kushindwa jamii ya kimataifa na taasisi husika katika kuzuia jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Palestina na Lebanon.

Kuanzia tarehe 7 Oktoba 2023, utawala wa Kizayuni ukiungwa mkono kikamilifu na nchi za Magharibi, ulianzisha mauaji makubwa ya kimbari katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya watu wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina ambapo kimya kikubwa cha jamii ya kimataifa, na taasisi za kutetea haki za binadamu katika kukabiliana na jinai za kinyama za  utawala huo ghasibu, kimepelekea kuendelezwa mauaji hayo dhidi ya wanawake na watoto wa Kipalestina.

Tangu kuanza mashambulizi hayo tarehe 7 Oktoba, Wapalestina 43,374 wameuawa shahidi na wengine 102,261 wamejeruhiwa.

Kadhalika, tangu tarehe 23 Septemba jeshi la Kizayuni limefanya mashambulizi makubwa katika maeneo mbalimbali ya kusini mwa Lebanon na kusababisha kuuawa shahidi zaidi ya watu elfu tatu.

Ayatullah Sayyid Ali Sistani, Marja Mkuu wa Mashia wa Iraq, ameeleza masikitiko yake makubwa katika mazungumzo yake na Mohammad al Hasan, Mkuu mpya wa Ujumbe wa Misaada ya Umoja wa Mataifa nchini Iraq (UNAMI), ambaye pia ni Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika nchi hiyo, na ujumbe alioandamana nao, kuhusu maafa ya sasa nchini Lebanon na katika Ukanda wa Gaza, na kusikitishwa sana na kushindwa jamii ya kimataifa na taasisi husika katika kuzuia uchokozi wa kinyama unaofanywa na utawala huo pandikizi.

Ayatullah Sistani pia, amesema: 'Wairaqi, hasa wasomi, wanapaswa kufanya kila wawezalo kushinda vikwazo na kufanya kazi kwa bidii ili kufikia mustakabali bora kwa manufaa ya nchi yao.'

Kwingineko katika mazungumzo yake, ameashiria changamoto zinazowakabili wananchi wa Iraq na kusema wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu wanapaswa kujifunza kutokana na tajiriba za huko nyuma na kujitahidi kufikia mustakbali mwema wa nchi hiyo ambayo kila mmoja ananufaika na utulivu, usalama, ustawi na maendeleo. Amesisitiza kuwa hilo halitawezekana bila kubuni mipango ya kiutendaji ya usimamizi wa nchi kwa uwazi na ufanisi.. Aidha alisisitiza haja ya kuzuia uingiliaji wowote wa kigeni katika masuala tofauti ya nchi.

4246317

Habari zinazohusiana
captcha