Katika hotuba yake ya pili ya hadhara tangu ashike uongozi siku ya Jumatano, Sheikh Qassem amesema harakati hiyo ya muqawama ya Lebanon imeazimia kuilazimisha Israel kuhitimisha vita vyake dhidi ya Lebanon, akieleza kuwa ni medani ya vita pekee ndiyo inayoweza kumaliza vita vinavyoendelea.
Amesema kuwa: "hakuna sehemu ndani ya "Israel" ambayo ndege zetu zisizo na rubani na makombora haziwezi kufika." “Hatutegemei uchaguzi wa Marekani, iwapo Harris atafaulu au Trump atashinda; hii haina thamani kwetu.”
Badala yake, alisema, Hizbullah iko tayari kuunda matokeo kupitia ushiriki wa kijeshi. Kwingineko katika hotuba yake amesema: "Maneno ya Shahidi Seyed Hassan Nasrullah ni nuru ya uongofu, na kama Imam Khamenei alivyosema kumhusu, hana mithili na mfano wake."
Sheikh Naim Qassem, amesema hayo katika hotuba aliyoitoa kwa mnasaba wa kumbukumbu ya Arubaini ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah aliyekuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah na kueleza kwamba, shahidi Nasrullah aliyaleta pamoja makundi yote ya jamii katika chama, kwa sababu Hizbollah ni chama cha watu huru, wapiganaji na watu wenye sharafu.
Amesema, sisi tunapingana vita vya kivamizi vya Israel dhidi ya Lebanon, na tunatoa salamu kwa pande za muqawama kutoka Yemen hadi Iraq na Lebanon, na kinara wao ni uungaji mkono mkubwa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC.
Amesema,vipengele vya nguvu za adui Mzayuni ni mauaji ya kimbari, mauaji ya raia, ukandamizaji, uvamizi na tabia za kishenzi. Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitiza kwa kusema: Tutawafanya Wazayuni waombe kusitishwa vita.
3490596