IQNA

Watu 28 wapoteza maisha katika mkasa wa moto bandari ya Shahid Rajaee, Iran

17:38 - April 27, 2025
Habari ID: 3480599
IQNA-Mkoa wa Kusini wa Hormozgan nchini Iran umetangaza siku tatu za maombolezo ya umma kufuatia mlipuko mbaya katika bandari ya Shahid Rajaee.

 

Gavana wa Hormozgan, Mohammad Ashouri Taziani, alitoa tangazo hilo Jumapili baada ya watu 28 kuuawa na zaidi ya wengine 1,000 kujeruhiwa kutokana na mlipuko mkubwa uliotikisa bandari ya makontena, iliyoko Bandar Abbas na inayoshughulikia tani milioni 80 za bidhaa kwa mwaka.
Mkuu wa Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Iran (IRCS), Pirhossein Koolivand, amesema kuwa watu 190 kati ya waliojeruhiwa bado wanapata matibabu. Ameongeza kuwa asilimia 90 ya moto tayari imezimwa na juhudi zinaendelea ili kuuzima kabisa ndani ya saa moja au mbili zijazo. Wakati huo huo, Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Mkoa wa Hormozgan, Mojtaba Ghahramani, amesema kuwa waathirika 10 kati ya waliokufa tayari wametambuliwa.W aziri wa Mambo ya Ndani wa Iran, Eskandar Momeni, amesema waokoaji kutoka mji mkuu Tehran na mikoa jirani ya Hormozgan wamesaidia katika shughuli za uokoaji.

Amebainisha kuwa maeneo yaliyoathiriwa na moto yamezingirwa ili kuzuia moto kuenea katika maeneo mengine ya karibu. Akizungumza Jumapili, Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, alisema kuwa ujumbe wa wabunge utatumwa Hormozgan kutoa ripoti ya kina kuhusu tukio hilo.Uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha mlipuko huo na kuzuia tukio kama hilo kutokea tena.

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umetuma salamu za pole kwa wananchi na serikali ya Iran kufuatia mripuko mkubwa uliotokea  katika bandari ya Shahidi Rajaee kusini mwa Iran jana Jumamosi.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema kuhusu mripuko uliotokea katika Bandari ya Shahid Rajaee huko Bandar Abbas, Iran: "Tumesikitishwa sana watu wengi walioathirika katika mripuko wa jana uliotokea katika Bandari ya Shahid Rajaee huko Bandar Abbas katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran". Dujarric amesema: Tunatoa pole  kwa familia za wahanga, wananchi na serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na tunawatakia afueni ya haraka majeruhi wote. 

3492845

Kishikizo: iran
captcha