IQNA

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq yasifu mafanikio ya mpango wa usalama wa Ashura Karbala

15:31 - July 07, 2025
Habari ID: 3480913
IQNA – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq imetoa taarifa mchana wa Jumapili ikitangaza mafanikio ya utekelezaji wa mpango wa usalama kwa ajili ya maombolezo ya mwaka huu ya Siku ya Ashura mjini Karbala.

Wizara hiyo ilisema kuwa sifa ya kipekee ya mpango wa usalama wa mwaka huu ilikuwa ni utekelezaji wake bila kutumia silaha yoyote.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa makumi ya maelfu ya wafanyaziara kutoka nje ya nchi walishiriki katika maombolezo ya Ashura mwaka huu, na shughuli za kuingia na kutoka ziliendeshwa kwa utaratibu na salama kabisa.

Miqdad Miri, mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Habari katika wizara hiyo, alieleza kuwa maombolezo ya mwaka huu ya Ashura yamekuwa miongoni mwa yaliyoandaliwa kwa nidhamu ya hali ya juu zaidi katika miaka ya hivi karibuni, ikiwemo mienendo ya wafanyaziara, hatua za kiusalama na utoaji wa huduma.

Afisa huyo alisisitiza kuwa mpango huo maalum wa kiusalama na kihuduma ulitekelezwa kwa ukamilifu kama ulivyopangwa, chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Waziri wa Mambo ya Ndani na kwa ushiriki wa moja kwa moja wa makamanda na maafisa wa vikosi vya usalama.

Wakati huohuo, Wizara ya Afya ya Iraq ilitangaza kuwa timu zake zimewahudumia zaidi ya waombolezaji milioni 12 wa Ashura kwa huduma za kitabibu, elimu ya afya na msaada wa dharura.

Wizara hiyo ilieleza kwamba pia kulikuwepo na vikosi vya kujitolea vilivyoshiriki kuwahudumia wafanyaziara waliohudhuria tukio la Rakdha Tuwairaj mjini Karbala kwa kutoa huduma za afya, elimu na misaada mbalimbali.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa wahudumu wa kujitolea hao walionyesha moyo wa kujitolea na sadaka kwa msingi wa wajibu wao wa kidini na kibinadamu kwa ajili ya wafanyaziara wa Imamu Hussein (AS), huku wakitoa pole zao za dhati kwa mashahidi wa Karbala.

Wizara hiyo ilisisitiza kuwa inatilia mkazo mkubwa utoaji wa huduma bora za afya katika matukio makubwa kama haya, kwa kuweka mikakati ya kinga na uratibu wa juu ili kuhakikisha afya ya wafanyaziara na utukufu wa ibada unahifadhiwa.

Waislamu wa Kishia, pamoja na wengine kutoka maeneo mbalimbali ya dunia, huadhimisha kila mwaka katika mwezi wa Muharram kumbukumbu ya kuuliwa shahidi kwa Imamu Hussein (AS) pamoja na maswahaba wake.

Imamu Hussein (AS), Imamu wa Waislamu wa Madhehebu ya Shia, pamoja na kundi dogo la familia yake na maswahaba wake, waliuawa shahidi katika vita vya Karbala mnamo tarehe 10 ya Muharram mwaka 61 Hijria sawa na 680 Miladia, mikononi mwa dhalimu Yazid bin Muawiya.

Mwaka huu, siku ya Ashura iliangukia Jumapili, tarehe 6 Julai 2025.

captcha