IQNA

Maulamaa wataka nchi za Kiislamu zikate uhusiano na Israel

23:47 - January 29, 2018
Habari ID: 3471375
TEHRAN (IQNA)-Nchi za Kiislamu zilizo na uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel zimetakiwa zikate uhusiano huo mara moja kama njia ya kuunga mkono ukombozi wa Palestina hasa mji wa Quds (Jerusalem).

Wito huo ni sehemu ya maazimio 14 yaliyopitishwa na wasomi watajika wa Kiislamu kutoka nchi zaidi ya 30 waliokuwa wakishiriki katika kikao cha "Jukwaa la Maulamaa wa Kiislamu Kuhusu Quds" huko Putrajaya nchini Malaysia.

Mratibu wa kongamano hilo Dr Mohd Khairuddin Aman Razali amesema wito huo umetolewa kutokana na nchi kadhaa za Kiarabu kuwa na uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.

"Njia ya kukomboa Msikiti wa Al Aqsa (ulio katika mji wa Quds) ni kupitia kukata uhusiano wa kisiasa, kibiashara, kiuchumi nk. Na utawala wa Kizayuni wa Israel.

"Iwapo nchi moja tu itachukua hatua hiyo, basi jambo hilo halitakuwa na athari sana," alisema katika mkutano na waandishi habari baada ya mkutano huo wa siku tatu ulioanza Ijumaa.

Maazimio hayo yantazamiwa kukabidhiwa Waziri Mkuu wa Malaysia Najib Abdul Razak ili ayakabidhi kwa viongozi wan chi za Kiislamu kwa ajili ya utekelezwaji.

Nchi za Kiarabu zilizo na uhusiano rasmi na Israel ni Misri na Jordan huku nchi kama vile Saudi Arabia, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu zikiwa na uhusiano wa siri na utawala huo  wa Kizayuni.

Halikadhalika kati ya maazimio ya kongamano hilo ni kuhakikisha kuwa kadhia ya Quds na Msikiti wa Al Aqsa inafundishwa katika shule za msingi na vyuo vya juu vya elimu katika nchi za Kiislamu ili vijana Waislamu waweze kuelimishwa kuhusu maeneo hayo kwani Mayahudi huwa wanawafunza watoto wao kuwa Quds ni mji wao.

Mwenyekiti wa Baraza la Kiislamu Syria Sheikh Usamah al-Rifa'I amesema iwapo wanazuoni wote wa Kiislamu na viongozi wataazimia kutekeleza maazimio hayo, basi hiyo itakuwa hatua ya kwanza katika kuikomboa Quds Tukufu.

3465071

captcha