Mehdi Rezazadeh Joudi, katika makala yake, ameeleza malengo ya kuanzishwa kwa bunge hilo, ikiwa ni pamoja na kuimarisha diplomasia ya Qur'ani kama njia madhubuti ya kukabiliana na changamoto za kimataifa.
Hujjatul Islam Mohammad Mehdi Imanipour, mkuu wa Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu (ICRO), alitoa pendekezo la kuanzisha bunge la Qurani la ulimwengu wa Kiislamu alipohutubia Kongamano la 20 la Kimataifa la Kiislamu mjini Moscow, Russia, Septemba 2024.
Hapa kuna muhtasari wa makala hiyo:
Katika kipindi ambacho Ummah wa Kiislamu unakabiliwa na migogoro ya utambulisho, kidini na kijiografia, kurejea kwenye misingi ya pamoja ni jambo lisiloweza kuepukika. Qur'ani, kama hati ya mwisho na msingi wa pamoja wa imani ya Waislamu, ina uwezo usiopingika wa kuchukua nafasi ya uongozi katika njia ya kuleta umoja wa Kiislamu.
Katika muktadha huu, kuanzishwa kwa bunge la Qur'ani la ulimwengu wa Kiislamu kunaweza kuonekana kama mkakati muhimu wa kushinda migogoro na kufikia lengo la kuwa na Ummah uliounganika.
Mpango huu, katika kipindi ambacho ulimwengu wa Kiislamu unakabiliwa na migawanyiko ya kijamii ya kina, unaweza kuwa taa ya mshikamano na ushirikiano kati ya nchi za Kiislamu. Kwa kuzingatia tofauti kubwa za kitamaduni na kidini miongoni mwa Waislamu, Qur'ani inaweza kuwa kiunganishi ambacho Waislamu wote duniani wanakikubali.
Katika muktadha huo, kuanzishwa kwa taasisi ya kimataifa inayoitwa Bunge la Qur'ani la Ulimwengu wa Kiislamu kunaweza kuunda fursa mpya za uratibu katika nyanja mbalimbali za kimataifa na kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha mawasiliano na kutatua matatizo ya pamoja.
Bunge hili litakuwa taasisi ya kimataifa itakayowaleta pamoja wawakilishi wa wafuasi wa madhehebu mbalimbali ya Kiislamu kwa misingi ya mafundisho ya Qur'ani.
Lengo la taasisi hii siyo kuleta mivutano juu ya tofauti za kidini, bali kuweka njia ya maendeleo, haki ya kijamii, udugu wa Kiislamu na kukabiliana na changamoto mpya za ulimwengu wa Kiislamu. Kuanzishwa kwa baraza kama hili kunaweza kutoa fursa muhimu za mazungumzo ya kujenga kati ya nchi mbalimbali za Kiislamu na kufungua njia za ushirikiano mkubwa katika masuala kama elimu, maendeleo, utamaduni na siasa.
Miongoni mwa majukumu muhimu ya bunge hili ni kueleza thamani za Qur'ani katika nyanja za siasa, utamaduni na jamii, kuandaa miswada ya umoja wa kukabiliana na migogoro ya ulimwengu wa Kiislamu, kutetea haki za mataifa ya Kiislamu yaliyodhulumiwa, na kupinga miradi ya kimataifa ya chuki dhidi ya Uislamu na ya kugawa Waislamu.
Mpango huu ni majibu ya wazi kwa amri ya Mwenyezi Mungu: “Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja wala msifarikiane.”
Lengo jingine la bunge la Qur'ani ni kukuza na kuimarisha diplomasia ya Qur'ani kama mbinu yenye ufanisi katika kukabiliana na changamoto za kimataifa.
Diplomasia ya Qur'ani inaweza kuchukua nafasi muhimu katika kupunguza mvutano na migogoro ya kisiasa, kijamii na kiuchumi katika nchi za Kiislamu. Pia, itarahisisha kufanyika kwa vikao maalum, kuandaliwa kwa tamko za pamoja, utekelezaji wa miradi ya kiutamaduni na ya vyombo vya habari inayozingatia Qur'ani, na uwasilishaji wa suluhisho za kutatua migogoro ya kikanda, ikiwa ni pamoja na hatua za vitendo za bunge hilo.
Inaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha mahusiano miongoni mwa Waislamu na kurahisisha mazungumzo ya pamoja ya kutatua matatizo ya kidunia.
Bunge la Qur'ani la ulimwengu wa Kiislamu linaweza kuwa na nafasi katika kurejesha mamlaka ya Waislamu katika ulingo wa kimataifa, huku likiimarisha mtaji wa kiroho na kiakili wa Ummah wa Kiislamu. Mamlaka haya, yanayopatikana kupitia utamaduni, vyombo vya habari na sera za pamoja, yanaweza kuwa na mchango muhimu katika kuimarisha nafasi ya Waislamu katika jukwaa la dunia na kuongeza mchango wao katika nyanja mbalimbali kama uchumi, sayansi na teknolojia, na siasa za kimataifa.
Utimilifu wa mpango huu wa kimkakati unahitaji uthabiti wa wasomi wa kidini, msaada wa wataalamu na wanazuoni, ushirikiano wa wanasiasa, na umoja wa nyoyo wa Ummah wa Kiislamu.
3492896