Ujumbe wa Iran ukiongozwa na Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Kueneza Qur'ani cha Shirika la Iran la Utamaduni na Uhusiano wa Kiislamu (ICRO) Hujjatul Islam Seyed Mostafa Hosseini Neyshabouri uko katika ziara nchini Malaysia ili kubainisha maeneo ya ushirikiano katika nyanja za Qur'ani na kidini.
Katika kikao na rais wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kiislamu cha Malaysia, Hujjatul Islam Hosseini Neyshabouri amesema ushirikiano unapaswa kupanuka kati ya nchi hizo mbili katika kuandaa utafiti wa Qur'ani na kubainisha na kuondoa matatizo na vikwazo.
Vile vile amesisitiza utayarifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuhuisha diplomasia ya Qur'ani kati ya nchi mbili za Kiislamu ambazo ni madola yenye taathira katika ulimwengu wa Kiislamu.
Afisa huyo wa Iran pia alibainisha kwamba kuibuka kwa ustaarabu wa Kiislamu kuliwezekana kutokana na mafundisho ya Qur'ani Tukufu na hakuna mtu anayeweza kupata kipengele chochote cha ustaarabu huu ambamo Kitabu Kitukufu hakijachukua jukumu muhimu.
Rais wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kiislamu cha Malaysia, kwa upande wake, aliukaribisha ujumbe wa Iran na kusisitiza kukuza ushirikiano wa Qur'ani kati ya Tehran na Kuala Lumpur.
Vile vile amesema kuainisha masomo ya Qur'ani ni muhimu ili kustawisha ushirikiano katika nyanja hii.
Pande hizo mbili pia zilijadili mbinu mpya za utafiti katika nyanja za Kiislamu na Qur'ani. Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kiislamu cha Malaysia kwa sasa kina zaidi ya wanafunzi 25,000 kutoka nchi 100.
3490382