Hujjatul Islam Mohsen Mohajernia, profesa wa chuo kikuu, mwalimu wa Hawza (chuo cha Kiislamu) na mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Mapinduzi ya Kiislamu cha Tolou-e-Mehr, amelitaja tukio hilo kama hatua ya hekima ya kisiasa iliyochukuliwa na Mtume Muhammad (SAW) katika wakati wa mivutano mikali.
“Waislamu walikuwa wametoka kwenye ushindi wa vita vya Khandaq, vita vilivyokuwa tishio kubwa zaidi kwa serikali changa ya Kiislamu, ambapo makabila yote ya Waarabu wapinzani waliungana kuangamiza Uislamu,” alisema Mohajernia. “Katika mazingira hayo tete, Mtume (SAW), akiwa ameonyeshwa ndoto ya kweli, aliongoza msafara wa Waislamu takriban 1,400 kwa nia ya kutekeleza Umrah, bila silaha na kwa ajili ya ibada tu.”
Hata hivyo, Quraysh waliwazuia Waislamu kuingia Makkah na kuwalazimisha kusimama eneo la Hudaybiyyah. “Ingawa baadhi ya Maswahaba walitamani mapambano, Mtume (SAW) alitumia hekima ya hali ya juu kugeuza mgogoro huo kuwa fursa ya kihistoria kwa kusaini mkataba wa amani wa miaka 10.”
Ingawa masharti ya awali yalionekana kuwa ya upendeleo kwa Quraysh, Mohajernia alieleza kwamba Mtume (SAW) alithibitisha uhalali wa uamuzi wake kwa kusimamisha upya kiapo cha utii, maarufu kama Bay‘at al-Ridwan. Alipokuwa njiani kurejea Madina, Allah aliteremsha Sura ya Al-Fath ("Ushindi") akitangaza:
“Hakika Tumekupa ushindi wa wazi kabisa” (Qur’an 48:1), jambo lililodhihirisha kuwa mkataba huo ulikuwa ni ushindi wa kimungu.
Mohajernia alibainisha faida kuu za kimkakati zilizotokana na mkataba huo:
1. Uhalali wa Serikali ya Kiislamu
Mkataba huo uliilazimisha Quraysh kuutambua mji wa Madina kama mamlaka halali ya kisiasa, na hivyo kuupa Uislamu heshima ya kimataifa kwa mara ya kwanza.
2. Usalama na Dira ya Diplomasia ya Kigeni
Mwisho wa vita ulifungua milango ya uenezi wa Uislamu kwa njia ya barua rasmi kwa watawala wa mataifa kama Uajemi, Byzantium, na Misri, waakialikwa kuingia katika Uislamu.
3. Taswira ya Uislamu Kimataifa
Waislamu hawakuonekana tena kama wapiganaji tu, bali kama wajumbe wa amani na mazungumzo ya busara, hali iliyowavunja nguvu kisaikolojia maadui wa Uislamu.
4. Wafuasi wapya kwa kasi kubwa
Katika kipindi cha miaka miwili baada ya mkataba, idadi ya watu walioingia Uislamu ilizidi idadi ya walioingia tangu mwanzo wa ujumbe wa Mtume (SAW), kwa mujibu wa wanahistoria wengi.
5. Mabadiliko ya Ndani
Mkataba huo ulifundisha Ummah kuwa ushindi unaweza kupatikana kwa njia ya mazungumzo, sio daima kwa upanga. Hii ilikuza fikra ya kisiasa na ustaarabu wa Kiislamu.
6. Ushindi wa Khaybar
Amani ya Hudaybiyyah ilitoa nafasi ya kulimaliza tishio la makundi ya Kiyahudi waliokuwa wakihujumu Uislamu. Hapa ndipo Imam Ali (AS) alipong’ara kwa kuteka Khaybar, ishara ya ujasiri wa Ummah dhidi ya maadui.
7. Kufunguka Njia ya Kukomboa Makkah kwa Amani
Mwisho, mkataba huu ulifungua mlango wa ushindi wa amani wakati wa kuchukua udhibiti wa mji wa Makkah, na kuthibitisha kuwa Mtume Muhammad (SAW) hakutaka vita wala uharibifu wa maeneo matukufu, bali alifuata mkakati wa muda mrefu na madhubuti.
“Hudaybiyyah inabaki kuwa mfano wa milele wa diplomasia ya heshima na mkakati katika historia ya Kiislamu,” alihitimisha Mohajernia.
4293586