
Amehifadhi Qur’ani Tukufu yote licha ya kuugua saratani ambayo imekuwa ikidhoofisha mwili wake kwa miaka kadhaa.
Safari ya Shorouk na Qur’ani ilianza miaka miwili iliyopita, mwanzoni mwa vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza, akivutiwa na wahifadhi wa Qur’an wa Gaza licha ya mateso wanayopitia.
“Niliona watu wa Gaza wakihifadhi Qur’an licha ya maumivu na mateso, nikajiambia: Ikiwa wao wanaweza, basi na mimi naweza,” alisema Shorouk, kwa mujibu wa Al Jazeera.
Alijitolea kubeba Qur’ani katika kila hatua ya matibabu yake ya muda mrefu dhidi ya saratani.
Katika korido za Hospitali ya Al-Mutala huko al-Quds inayokaliwa kwa mabavu, alihifadhi aya wakati akisubiri vipindi vya tiba ya mionzi, akitumia saa za kusubiri kusoma, kurudia na kuhifadhi.

Shorouk, mama wa watoto watatu, hakukata tamaa kwa sababu ya ugonjwa huo, bali mateso ya saratani yakawa msukumo wa kuendelea na njia mpya ya ukaribu na Qur’ani Tukufu.
Anasema: “Hakuna kinachotuliza moyo kama aya za Qur’ani, na hakuna tiba ya kina kwa roho kama aya zake. Nawashauri wote wanaopitia hali ngumu waichukue Qur’ani kama dawa yao na rafiki wa kudumu.”

Akram Dawood, mama yake Shorouk, hakuweza kujizuia kulia alipogundua kuwa binti yake amekamilisha kuhifadhi Qur’ani Tukufu.
Anasema: “Shorouk aliponiambia kuwa amehifadhi Qur’ani yote, nililia kwa furaha. Hii ni zawadi nzuri zaidi niliyopata maishani.”
Anaongeza: “Nilikuwa nikimtia moyo kila wakati licha ya hali ngumu aliyokuwa nayo, na namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumsaidia na kumwongoza.”
4314943