IQNA

Mashindano ya Qur’ani kwa wenye ulemavu wa macho yafanyika Kuwait

12:27 - November 13, 2025
Habari ID: 3481507
IQNA – Mashindano ya kwanza ya kitaifa ya Qur’ani kwa watu wenye ulemavu wa macho nchini Kuwait yamefanyika kwa juhudi za Taasis ya Mutamayizin kwa Huduma ya Qur’ani.

Mashindano hayo yaliandaliwa kwa kauli mbiu “Mwanga wa Nyoyo” yakihusisha washiriki 120 wenye ulemavu wa macho, gazeti la Al-Rai linaripoti.

Lengo kuu lilikuwa ni kuunga mkono ushiriki wa watu wenye ulemavu katika shughuli za Qur’ani na kuimarisha nafasi yao katika jamii.

Kwa mujibu wa Yousef Al-Samiei, mwenyekiti wa baraza la utawala la Taasis ya Mutamayizin, watu wenye ulemavu ni sehemu muhimu ya jamii.

“Daima tunajitahidi kuwasaidia na kuwapatia nafasi ya kushiriki katika shughuli mbalimbali,” alisema.

Aliongeza kuwa shule za elimu binafsi, Chuo Kikuu cha Kuwait, Idara Kuu ya Elimu ya Vitendo, Jumuiya ya Wasioona na Klabu ya Al-Basira ziliungana kushirikiana katika kufanikisha mashindano hayo.

Al-Samiei alibainisha kuwa mshikamano wa taasisi hizo unaonyesha juhudi za pamoja za kuweka mazingira muafaka kwa uwepo wa wenye uoni hafifu katika jamii na kuonyesha uwezo wao wa kuhifadhi Qur’ani Tukufu.

Washiriki 120 kutoka makundi mbalimbali ya umri walihudhuria mashindano haya. Aidha, alieleza kuwa makundi kadhaa yameundwa kwa lengo la kupanua ushiriki na kutoa nafasi kwa idadi kubwa zaidi ya wahifadhi wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu kushiriki.

Sherehe ya kufunga mashindano haya, ambapo washindi watatunukiwa heshima, imepangwa kufanyika chini ya usimamizi wa waziri wa masuala ya kijamii wa Kuwait mnamo tarehe 6 Disemba 2025.

3495361

captcha