IQNA

19:35 - October 16, 2021
News ID: 3474429
TEHRAN (IQNA)- Mkutano wa 35 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu utafanyika Tehran na kushirikisha wasomi 50 maarufu duniani.

Hayo yamesemwa na Hujjatul Islam Hamid Shahriari, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu amesema kongamano hilo la kila mwaka litaanza Oktoba 19.

Amesema kutokana na kuendelea janga la COVID-19, imeamuliwa kuwa idadi ya washiriki iwe ndogo na katika kiwango cha Mamufti na wanazuoni pamoja na wasomi wa ngazi za juu wa ulimwengu wa Kiislamu.

Halikadhalika amesema kuna idadi kubwa ya  wanazuoni na  wanaharakati watakaoshiriki katika kongamano hilo kwa njia ya intaneti.

Hujjatul Islam Hamid Shahriari amesema kauli mbiu ya kongamano la mwaka huu ni, “Umoja wa Kiislamu, Amani na Kuzuia Mifarakano na Mizozo katika Ulimwengu wa Kiislamu.”

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu amesema kwa kuzingatia masaibu ya ulimwengu wa Kiislamu kama vile vita, umwagaji damu na ugaidi, kikao cha mwaka huu pia kitajadili mada nyingine muhimu ya ‘Vita na Amani Yenye Uadilifu’. Mada zingine zitakazpewa umuhimu ni pamoja na Palestina na Mapambano ya Kiislamu, Udugu wa Kiislamu, Kukabiliana na Ugaidi, Kuheshimiana  Wafuasi wa Madehebu za Kiislamu, Umma Moja, na Muungano wa Nchi za Kiislamu.

Hujjatul Islam Hamid Shahriari amesema kongamano hilo la siku sita litahutubiwa na Rais wa Iran na pia Spika wa Bunge la Iran.

Kongamano la mwaka jana la kimataifa la umoja wa Kiislamu lilifanyika kwa njia ya intaneti kutokana na janga la COVID-19.

Mkutano huo hufanyika kila mwaka kwa munasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu. Inafaa kuashiria hapa kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni kipindi cha kati ya tarehe 12 na 17 za Mfunguo Sita Rabiu Awwal kipindi ambacho kinasadifiana na kuadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Bwana Mtume SAW. Kuhusiana na kuzaliwa Bwana Mtume SAW kuna riwaya mbili mashuhuri. Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisuni wanaamini kwamba, Bwana Mtume SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia.

Kundi jengine la Waislamu ambalo linaundwa zaidi na Waislamu wa madhehebu ya Shia Ithanaashari linaamini kwamba, Mtume wa Uislamu alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka huo huo. Mitazamo hiyo miwili takribani pengo lake ni kipindi cha wiki moja. Kwa kuzingatia hali hiyo, Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini (MA) Mwasisi na Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akakitaja kipindi hiki cha wiki moja kuwa Wiki ya Umoja, ili Waislamu badala ya kuvutana na kuanza kukuza tofauti za tarehe za kuzaliwa Bwana Mtume SAW wakae pamoja na kujadili umuhimu wa umoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili Waislamu na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla.

4005214

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: