IQNA

Waislamu waanza kufunga katika baadhi ya nchi, nyingine zatangaza kuanza kwa Ramadhani Alhamisi

9:54 - February 18, 2026
Habari ID: 3481952
IQNA — Wakati baadhi ya nchi za Kiarabu zimetangaza Jumatano kuwa siku ya kwanza ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Waislamu katika mataifa mengine mengi wataanza kufunga Alhamisi.

Leo ni siku ya kwanza ya Ramadhani katika baadhi ya nchi za Kiarabu, zikiwemo Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Qatar, kwa mujibu wa ripoti ya Al‑Sharq.

Nchi hizo tatu zilithibitisha Jumanne jioni kuwa mwezi mtukufu umeanza tarehe 18 Februari.

Hata hivyo, nchi kadhaa barani Asia, Mashariki ya Kati na Afrika zimetangaza Alhamisi, tarehe 19 Februari, kuwa siku ya kwanza ya Ramadhani.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kituo cha Kimataifa cha Astronomia, kuonekana kwa hilali ya Ramadhani jioni ya Jumanne, tarehe 17 Februari 2026, hakukuwa kunawezekana au kulionekana kuwa kugumu sana katika sehemu kubwa ya ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu, iwe kwa macho ya kawaida, kwa kutumia darubini, au hata kwa teknolojia za kisasa za upigaji picha za kiastronomia.

Nchi zingine kama vile Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Uturuki Oman, Jordan, Syria,  Misri,  Indonesia na Bangladesh zimetangaza kwamba kesho Alkhamisi ndiyo mwanzo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Katika eneo la Afrika Mashariki, Kaimu Kadhi Mkuu wa Kenya, Sheikh Sukyan Omar ametangaza jana kutoonekana kwa mwezi mwandamo na hivyo Alhamisi itakuwa siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani nchini humo. Hatahivyo Msikiti wa Jamia jijini Nairobi umetangaza kufuata tangazo la Saudi Arabia na hivyo kupinga kauli ya Kaimu Kadhi mkuu wa nchi hiyo.

Nchini Tanzania, Sheikh Khamis Said Mataka mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) ametangaza kuwa mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan unatarajiwa kuanza kesho February 19 kwa mujibu wa mwandamo wa mwezi.

Baadhi ya wanazuoni wa dini hutegemea hesabu za kiastronomia kubaini mwanzo wa miezi ya Hijria, ilhali wengi wao wanasisitiza kuwa kuonekana kwa macho ya hilali ndiko kunakopaswa kuzingatiwa katika suala hili.

Ramadhani ni mwezi wa tisa na wenye utukufu mkubwa zaidi katika kalenda ya Kiislamu, ambapo Waislamu hukumbuka kushushwa kwa Qur’ani Tukufu kwa Mtume Muhammad (rehema na amani ziwe juu yake).

Katika mwezi huu mtukufu, Waislamu hufunga kuanzia alfajiri hadi machweo ya jua, wakijizuia kula, kunywa na yote yaliyokatazwa katika mwezi huu mtukufu. Aidha, huongeza juhudi katika swala, sadaka na matendo mema, wakitafuta kuimarisha imani yao na kutakasa nyoyo zao mbele ya Mwenyezi Mungu.

Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) linawatakia Waislamu wote ulimwenguni Ramadhani Mubarak na funga njema pamoja na kutakabaliwa Saumu na ibada zao katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

3496454

captcha