IQNA

Rais wa Pezeshkian: Iran haina nia ya kuzozana na nchi za Kiislamu

15:00 - March 21, 2026
Habari ID: 3482078
IQNA-Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ametoa ujumbe maalumu kwa mnasaba wa mwaka mpya wa Kiirani wa Hijria Shamsia, 1405 na kusema Iran haina nia ya kuzozana na nchi za Kiislamu na kuongeza kuwa: “Mwaka huu, kuliko wakati mwingine wowote, tunaihitaji Nowruz; Nowruz inayonyesha umoja kwa dunia.”

owruz ni jina la sikukuu ya mwaka mpya katika kalenda ya Kiirani.

Masoud Pezeshkian amesema katika ujumbe wake wa Nowruz siku ya Ijumaa kwamba: “Mwaka huu matukio mawili yenye baraka yamekutana pamoja; moja ni Nowruz na jingine ni Eid al‑Fitr. Nowruz, katika utamaduni na imani yetu, kwa karne na milenia nyingi imekuwa ikizingatiwa kuwa mwanzo mpya wa maisha katika nchi yetu.”

Rais wa Iran amesema: “Hatuna nia ya kuwa na migongano na nchi za Kiislamu. Hatutaki mzozo wala vita na mataifa ya Kiislamu; wao ni ndugu zetu. Mivutano iliyopo inachochewa na adui mwenye nia mbaya ambaye kwa mbinu na mwenendo wake husababisha matatizo miongoni mwetu sisi Waislamu na ndani ya jamii zetu.”

Rais Pezeshkian ameongeza: “Katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, walimuua shahidi kiongozi wetu mpendwa bila sababu wala mantiki. Pia waliua shahidi makamanda wetu na mawaziri wetu bila sababu wala mantiki.”

Ameendelea kusema: “Watoto 168 wasio na hatia waliuawa shahidi katika shule ya msingi. Mabegi yao ya mgongoni yalikuwa yamejaa matumaini na ndoto walizotaka kuishi nazo. Hawa ndio wanaodai ubinadamu na kujigamba mbele yetu kuwa ni watetezi wa haki za binadamu.”

Amesisitiza kwamba: “Hatukuwahi kufuatilia silaha za nyuklia kwa namna yoyote. Kila tulipokutana na Kiongozi Muadhamu na wajumbe wa Baraza Kuu la Ulinzi pamoja na makamanda, alisisitiza wazi kuwa silaha za nyuklia ni haramu kwa misingi ya dini ya Kiislamu.”

Ameongeza kuwa: “Hata hivyo, Marekani na rais wake wanaijengea dunia taswira kwamba sisi tulikuwa na nia ya kuelekea kwenye silaha za nyuklia. Kwa bahati mbaya, vyombo vingi vya habari duniani vinakubali madai hayo na kuripoti kwa msingi wa taarifa hizo.”

Rais Pezeshkian amekumbusha kuwa: “Tunataka kukabiliana na wale waliovuruga utulivu katika eneo hili. Walidhani kwamba kama kiongozi wetu mpendwa atauawa shahidi, na makamanda wetu pia, mshikamano wa nchi ungesambaratika.”

Rais Pezeshkian ameashiria madai ya Rais wa Marekani aliyedai kwamba: ‘Maandamano  ya wananchi wa Iran si ya kweli na picha zilizopo ni za akili mnemba na kusema: "Ni vyema awatume waandishi wake wa habari waje waone jinsi ‘akili hii mnemba’—inayotembea na kupaza sauti—inasimama kutetea ubinadamu, haki, watu na heshima ya nchi yake.”

Rais wa Iran aidha amesema: “Majirani zetu wapendwa wanaoizunguka Iran, ninyi ni ndugu zetu. Matatizo au madhara yoyote yaliyotokea katika mahusiano yetu, tunaomba Mwenyezi Mungu atusaidie kuyatatua. Tuko tayari kutatua matatizo yote pamoja nanyi, ndugu zetu wapendwa.”

Ameendelea kwa kusema: “Pendekezo letu ni kuunda muundo wa usalama unaotokana na nchi za Kiislamu za Mashariki ya Kati ili kuhakikisha amani, usalama na utulivu katika eneo hili, kwa lengo la kuleta utulivu na maelewano.”

Rais wa Iran ameongeza kuwa: “Hatuhitaji uwepo wa wageni katika eneo hili. Tunaweza kuunda ‘Baraza la Kiislamu la Mashariki ya Kati’ kwa ushirikiano wa nchi za Kiislamu, na ndani ya mfumo huo tunaweza kupanga na kusimamia mahusiano yetu ya kiusalama, kiuchumi, kitamaduni na kisiasa.”

Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa: “Hatuna kabisa nia ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine. Hatutaki kabisa usalama na amani ya eneo hili uvurugike. Tunaweza kuyatatua haya sisi wenyewe, kwa kusaidiana na kushirikiana bega kwa bega. Huu ni ujumbe kwa nchi za eneo hili: Badala ya kueneza propaganda katika vyombo vya habari na kuwajulisha wananchi wenu kwamba Iran ndiyo chanzo cha machafuko ya eneo hili, ni bora mtambue na kuelewa kwamba Israel ndiyo chanzo cha vurugu, machafuko, mauaji ya halaiki, ugaidi na hujuma katika eneo hili.”

4342130

captcha