
Ayatullah Sayyid Mojtaba Hosseini Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika ujumbe wake kwa mnasaba wa kuanza mwaka mpya wa 1405, alitoa hoja na maelekezo kadhaa.
Matini ya ujumbe huo ni kama ifuatavyo:
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
Ewe Mgeuzaji wa nyoyo na macho,
Ewe Mpangaji wa usiku na mchana,
Ewe Mbadilishaji wa mambo na hali;
Ibadilishe hali yetu iwe katika hali iliyo bora zaidi.
Mwaka huu, majira ya kuchipua ya kiroho na ya kimaumbile , yaani Sikukuu Tukufu ya Idd al‑Fitr na sikukuu ya kale ya Nowruz, zimekutana kwa wakati mmoja. Kwa mnasaba huu, ninawapongeza wananchi wote mmoja baada ya mwingine kwa sikukuu hizi mbili za kidini na kitaifa, na hasa ninawapongeza Waislamu wote duniani kwa Idd al‑Fitr.
Vilevile, ninaona ni wajibu kutoa pongezi kwa ushindi mkubwa uliopatikana na wapiganaji wa Uislamu. Aidha, kwa familia zote na walioachwa na mashujaa waliouawa shahidi katika Vita vya Pili vya Kulazimishwa, jaribio la mapinduzi la mwezi wa Dey, Vita vya Tatu vya Kulazimishwa, pamoja na mashahidi wa usalama, walinzi wa mipaka na askari wasiojulikana waliotoa maisha yao, ninatoa salamu za pole na mshikamano wangu wa dhati.
Kwa mnasaba wa kuwasili kwa mwaka wa 1405 Hijria Shamsia, nina maelezo kadhaa ambayo napenda kuyawasilisha kama ifuatavyo.
Kwanza kabisa, nitafanya mapitio mafupi ya baadhi ya matukio muhimu ya mwaka uliopita. Katika mwaka uliopita, wananchi wetu wapendwa walikabiliwa na vita vitatu vya kijeshi na kiusalama. Vita ya kwanza ilikuwa ile ya mwezi wa Juni, ambapo adui wa Kizayuni, kwa msaada mahsusi wa Marekani na wakati mazungumzo yalipokuwa yakiendelea, alifanya shambulizi la kinyama na lisilo la haki. Katika shambulizi hilo, baadhi ya makamanda bora zaidi wa nchi na wanazuoni mashuhuri waliuawa shahidi, na baadaye takribani wananchi 1000 wa nchi yetu pia walipoteza maisha yao kwa daraja la ushahidi.
Kwa sababu ya kosa kubwa katika makadirio yake, adui alidhani kwamba baada ya siku moja au mbili tu, wananchi hawa wenyewe wangesimama na kuuangusha mfumo wa Kiislamu. Hata hivyo, kwa uangalifu na utambuzi wenu ninyi wananchi, pamoja na ushujaa usio na mfano wa wapiganaji wa Uislamu na kujitolea kwao kwa hali ya juu, kwa haraka sana dalili za udhaifu na kufedheheka zilianza kuonekana kwa upande wake. Hatimaye, kupitia upatanishi na juhudi za kusitisha mapigano, alijinasuasua na kujiepusha na hatari iliyokuwa ikimkabili.
Vita ya pili ilikuwa jaribio la mapinduzi ya mwezi Disemba, ambapo Marekani na utawala wa Kizayuni, walidhani kuwa wananchi wa Iran, kutokana na matatizo ya kiuchumi ya kulazimishwa, wangeitikia matakwa ya adui. Maadui walitumia vibaraka wao na kusababisha maafa mengi. Katika tukio hilo, idadi kubwa zaidi ya wananchi wetu wapendwa walipoteza maisha na kupata hadhi ya shahidi ikilinganishwa na vita iliyotangulia, na pia madhara makubwa yakapatikana katika sehemu mbalimbali za nchi.
Vita ya tatu ni vita ambayo kwa sasa tuko katikati yake. Katika siku yake ya kwanza, tulimsindikiza kwa macho yenye machozi na nyoyo zilizojeruhiwa baba mpendwa wa umma, Kiongozi wetu mtukufu, Mwenyezi Mungu ainue daraja lake tukufu, ambaye kwa shauku kubwa alikuwa akiongoza msafara wa mashahidi katika safari ya mbinguni kuelekea mahali palipoandaliwa kwa ajili yake chini ya kivuli cha rehema ya Mwenyezi Mungu, karibu na nuru za watakatifu, pamoja na kundi la wakweli (Sidiqqin) na mashahidi.
Tangu siku hiyo pia, polepole tuliendelea kuwaaga mashahidi wengine wa vita: miongoni mwao ni wanafunzi wa shule ya Shajaratu Tayyiba ya Minab, mabaharia mashujaa na waliodhulumiwa wa manowari ya Dena, makamanda na wapiganaji waliouawa shahidi kutoka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Jeshi la Iran (Artesh), Idara ya Polisi, jeshi la kujitolea la wananchi, Basij, askari wasiojulikana (idara za intelijensia), walinzi jasiri wa mipaka, na pia wananchi wengine wa taifa hili, wadogo kwa wakubwa, waliopita mbele yetu kama msafara wa nuru, nasi tukawaaga kwa huzuni na majonzi makubwa.
Vita vya sasa vilianza baada ya adui kukata tamaa ya kuona harakati kubwa ya wananchi ikiunga mkono upande wake. Kwa dhana potofu, alifikiri kwamba ikiwa ataua shahidi viongozi wa juu wa mfumo na baadhi ya watu wenye athari katika uongozi wa kijeshi, angeweza kuwatia hofu na kukata tamaa nyinyi wananchi wapendwa, na hivyo kuwafanya mjiondoe katika uwanja wa mapambano; na kwa njia hiyo kutimiza ndoto yake ya kutawala Iran na hatimaye kuigawanya vipande vipande.
Hata hivyo, katika mwezi huu mtukufu, mkiambatanisha saumu yenu na jihadi, na mkaunda mstari mpana wa ulinzi unaoenea kote nchini, pamoja na ngome madhubuti katika kila uwanja, mitaa na misikiti. Kwa njia hii mlimpa adui pigo la kumchanganya kiasi cha kumfanya aingie kwenye kauli zinazokinzana na maneno yasiyo na mashiko na hii ni dalili ya kukosa umakini na udhaifu wa utambuzi.
Kabala ya haya, tarehe 12 Januari ( 22 Dey), mlizima jaribio la mapinduzi, na tarehe 11 Februari (22 Bahman ) kwa mara nyingine mlionyesha msimamo wenu dhidi ya ubeberu wa kimataifa na kutokuchoka kwenu. Kisha tarehe 13 Machi (22 Esfand), ambayo ilikuwia sambamba na Siku ya Kimataifa Quds, kwa kumpa adui pigo lingine mlionyesha wazi kwamba adui hakabiliani tu na makombora, ndege zisizo na rubani, torpedo au masuala ya kijeshi pekee. Mstari wa mbele wa Iran ni mpana mno kuliko fikra yake ndogo na iliyodhalilika.
Ni wajibu wangu, katika hatua hii, kutoa shukrani za dhati kwa kila mmoja wa wananchi wetu wapendwa kwa kuunda tukio hili kubwa la kihistoria. Vilevile, nawapongeza rais jasiri, mwaminifu na wa watu, pamoja na maafisa wengine ambao katika hafla hizi walihudhuria miongoni mwa wananchi bila urasimu. Kitendo hiki chenyewe, na namna kilivyoonyeshwa, ni jambo lenye thamani kubwa ambalo linaweza kuimarisha zaidi mshikamano kati ya taifa na viongozi wake.
Kwa sasa, kutokana na umoja wa ajabu uliojitokeza miongoni mwenu, pamoja na kuwepo toofauti za kijamii, kijinsia, kiutamaduni, kiitikadi na kisiasa, ufa mkubwa umejitokeza ndani ya adui. Hii ni neema mahsusi kutoka kwa Mola Mtukufu, na inafaa kushukuriwa kwa ulimi, kwa moyo na pia kwa vitendo.
Miongoni mwa kanuni zisizokiukwa ni hii: neema yoyote inaposhukuriwa, mizizi yake huwa imara zaidi kwa kiwango cha shukrani iliyotolewa, au neema hiyo hupandishwa cheo, na baraka zaidi humiminika kwa yule anayeishukuru.
Kile ambacho kwa sasa kinahitajika katika kutekeleza shukrani kwa vitendo ni hiki: tuutambue umoja huu mkubwa kama rehema iliyo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na Mtukufu, na tujitahidi kadiri tuwezavyo kuutumia vyema. Kwa kufanya hivyo, mshikamano huu bila shaka utakuwa imara zaidi na wenye nguvu kama chuma, na maadui zenu watakuwa wanyonge na wenye kudhalilika zaidi.
Haya yalikuwa ni mapitio mafupi ya baadhi ya matukio muhimu ya mwaka 1404 Hijria Shamsia.
Sasa, tunapoingia mwaka 1405 Hijria Shamsia, tunakutana na mambo kadhaa. Kwanza, tunamuaga mgeni wetu mpenzi, mwezi mtukufu wa Ramadhani 1447 Hijria Qamaria, kwa mara ya mwisho. Katika mwezi huu, hasa katika Laylatul‑Qadr, nyoyo zenu zilielekezwa kwenye ulimwengu wa juu, mkamwita Mola Mwingi wa rehema, naye pia akakuelekezeni mtazamo wa huruma Yake.
Mlimuomba Bwana wetu – Mwenyezi Mungu Aharakishe Kudhihiri Kwake — na Mola Wake ushindi, afya, faraja na aina mbalimbali za neema. Na bila shaka, kwa kuzingatia historia ya hifadhi na fadhila ambazo daima zimeandamana na umma huu na mfumo huu, Inshaallah mtapokea ama kile kilicho katika vilindi vya nyoyo zenu au hata kilicho bora zaidi.
Wakati huohuo wa kuaga mwezi huu mtukufu, ambao uchungu wake huwa mkubwa zaidi kadiri ufahamu wa mtu unavyoongezeka , tunaukumbatia mwandamo mwema na wenye baraka wa Shawwāl al‑Mukarram, tukisubiri kwa hofu na matumaini zawadi ya Iddi kutoka kwa Mola Mtakatifu na Mwenye Kubariki.
Natumai kwamba baada ya zile ibada zenu za usiku na mchana zenye utambuzi wa wajibu, na baada ya kuifanya Siku ya Quds kuwa tukio la kifakhari, Mola Mtukufu atatutendea kwa wema, ustahamilivu, msamaha na upole mpana ambao tumeuzowea kutoka Kwake. Na hasa tunatumaini kwamba hivi karibuni, kwa bishara ya kufunguka kwa jambo kuu la kudhihiri kwa wazi kwa Bwana wetu, Hadhrat Waliyyullah al‑Aʿẓam, moyo wake mtukufu utajazwa furaha na bashasha; na kutokana na hilo, aina mbalimbali za baraka zitashuka juu ya watu wa dunia, kwa fadhila na ukarimu wa Mwenyezi Mungu.
Jambo jingine tunalokabiliana nalo ni tukio muhimu la sikukuu ya kale ya Nowruz. Sikukuu ambayo huja ikiwa imebeba zawadi kutoka kwa maumbile, zawadi ya upya, uhai na urindimo wa maisha, na ambayo kiasili inahusiana na furaha na bashasha.
Kwa upande mwingine, kwa wananchi wengi huu ni mwaka wa kwanza ambao Kiongozi wetu aliyeuawa shahidi pamoja na mashahidi wengine watukufu hawapo miongoni mwetu. Hasa nyoyo za familia na waliobaki nyuma ya mashahidi hawa bado zina huzuni na majonzi ya kuwapoteza wapendwa wao.
Kwa wakati huohuo, mimi binafsi , kama raia wa kawaida ambaye pia nimepoteza mashahidi kadhaa miongoni mwa watu wa karibu , ninaona kwamba pamoja na kuvaa mavazi ya maombolezo na kuwa na nyoyo zilizojaa huzuni kwa ajili ya mashahidi wote, bado tunafurahi sana kuona katika siku hizi wanandoa wapya wakiingia kwenye maisha yao mapya ya ndoa. Inshaallah dua ya Kiongozi wetu aliyeuawa shahidi pamoja na mashahidi wakubwa wa vita hii iwe pamoka nao na kuwabariki katika safari yao.
Nashauri pia kwamba wananchi kwa ujumla wakutane na watembeleana kama kawaida za siku hizi za mwaka, lakini kwa kuheshimu familia za mashahidi na kuzingatia hali yao. Na huenda watu wa kila mtaa, iwapo kutakuwepo uratibu unaofaa, wakaamua kuanza ziara zao za mwaka mpya kwa kuwatembelea na kuwatukuza mashahidi wa eneo lao.
Bila shaka, kipindi cha maombolezo ambacho serikali tukufu imepanga kwa ajili ya msiba wa kuuawa shahidi kwa Kiongozi wetu mpendwa kitasalia kama kilivyo, na kuheshimu kipindi hicho ni sehemu ya utukufu na hadhi ya mfumo huu na nchi hii.
Baada ya maneno haya, kuna maelezo mafupi mengine ya kuwasilisha.
Kwanza, napenda kutoa shukrani maalum kwa wale ambao katika siku hizi, pamoja na kuwepo kwao katika medani mbalimbali, mitaa na misikiti, wameongeza juhudi zao na kufanya nafasi yao ya kijamii ionekane zaidi. Miongoni mwao wapo baadhi ya vitengo vya uzalishaji, iwe vya serikali au vya sekta binafsi, pamoja na baadhi ya wafanyabiashara na watoa huduma. Kwa namna ya pekee pia nawataja wale watu ambao, bila hata kazi zao kuwalazimu kufanya hivyo, wanatoa huduma mbalimbali zenye manufaa kwa wananchi bila malipo. Alhamdulillah, aina hii ya watu wema na wenye kujitolea ipo kwa wingi.
Pili, mojawapo ya njia ambazo adui hutumia ni operesheni za vyombo vya habari. Katika kipindi hiki hasa, juhudi hizo zinalenga akili na nafsi za baadhi ya wananchi, kwa nia ya kudhoofisha umoja wa kitaifa na, kwa kufuatia hilo, kuathiri usalama wa taifa. Ni wajibu wetu kuwa waangalifu ili tusije, kwa uzembe wetu wenyewe, tukasaidia kutimia kwa azma hiyo ovu.
Kwa msingi huo, nasihi vyombo vya habari vya ndani ya nchi yetu, licha ya tofauti za fikra, mitazamo ya kisiasa na ya kitamaduni ambazo zinaweza kuwapo, vijiepushe kwa umakini mkubwa na kujikita katika kuonyesha au kukuza udhaifu. Vinginevyo, kuna uwezekano wa adui kufikia lengo lake.
Tatu, mwanya mmoja wa matumaini kwa adui ni kutumia m udhaifu wa kiuchumi na ya kiutawala ambao umekuwepo tangu zamani. Kiongozi wetu shahidi—Allah amwinue daraja yake—katika miaka tofauti alikuwa akielekeza mhimili mkuu na kaulimbiu ya mwaka kwenye masuala ya uchumi.
Kwa maoni yangu duni, kudhamini maisha ya wananchi, kuimarisha miundombinu ya kimaisha na ustawi, pamoja na kuzalisha utajiri kwa ajili ya umma, ni nukta kuu na aina fulani ya ulinzi, na hata hatua kubwa ya kusonga mbele dhidi ya vita vya kiuchumi vilivyoanzishwa na adui.
Miongoni mwa taufiki nilizopata ni fursa ya kusikiliza maneno ya wananchi wapendwa kutoka matabaka mbalimbali ya kijamii. Kwa mfano, katika kipindi fulani, nilikuwa nikisafiri nanyi mitaani mwa Tehran kwa sura nisiyofahamika ndani ya taksi niliyokuwa nimeiandaa kwa ombi langu mwenewe, nikitega masikio kusikiliza mazungumzo yenu. Niliiona njia hii ya kukusanya maoni kuwa ni bora zaidi kuliko kura nyingi za maoni za kitaalamu.
Katika visa vingi, mtazamo wangu uliendana na kauli zenu ambazo mara nyingi zilikuwa zikitolewa kama ukosoaji wa nyanja mbalimbali za kiuchumi na kiusimamizi. Katika mchakato huo, nilijifunza mengi kutoka kwenu, na bado ninaendelea kutafuta mafunzo mapya.
Hakika, katika kipindi hiki kabla na baada ya tarehe 19 ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, nilijifunza tena mambo mbalimbali kutoka kwenu, kwa kuwa mlikuwa mmejitoa na kuhudhuria katika medani mbalimbali. Natumai sitanyimwa neema hii.
Kufuatia masomo haya, kusikiliza haya, na tafiti zingine, jitihada zimefanywa kutunga rasimu ya tiba yenye ufanisi na iliyofanyiwa utafiti wa kitaalamu, ambayo kwa kadri inavyowezekana imekuwa ya kina na yenye pande nyingi. Alhamdulillah, hili limefanikiwa kwa kiwango kinachokubalika, na hivi karibuni itakuwa tayari kwa utekelezaji na viongozi wenye dhamira kubwa kwa ushirikiano wa wananchi wote, Inshallah.
Na mwishowe, katika sehemu hii, nikifuata njia ya kiongozi muadhamu shahidi, ninatangaza kauli mbiu ya mwaka huu kuwa ni: “Uchumi wa Kimuqawama (Kimapambano) unaojengwa kwa umoja wa kitaifa na usalama wa taifa.”
Nne, na hatimaye, lile nililotaja katika tamko langu la kwanza kuhusu mtazamo na sera ya mfumo wetu kuhusiana na mahusiano na nchi jirani ni jambo la kweli na la kutiliwa maanani.
Mbali na kipengele cha ujirani, tunashirikiana pia katika mambo mengine ya kiroho na kiutamaduni, miongoni mwa yote, imani yetu ya pamoja katika dini tukufu ya Uislamu, pamoja na kuwepo kwa makaburi matukufu na maeneo ya kipekee ya kidini katika baadhi ya nchi hizo. Aidha, Wairani wengi wanaoishi au kufanya kazi katika baadhi ya nchi jirani, na vilevile nukta za pamoja za kijamii, kidugu, au lugha moja, pamoja na maslahi ya kimkakati ya pamoja, hasa katika kukabiliana na kambi ya ubeberu duniani.
Kila kipengele kati ya hivi, kwa nafasi yake, kinaweza kuwa nguzo ya kuimarisha uhusiano mwema kati yetu na majirani wetu.
Miongoni mwa majirani zetu, tunawahisi wa mashariki kuwa karibu sana nasi. Mimi, kwa muda mrefu, nilikuwa najua kuhusu Pakistan kwamba ni nchi iliyokuwa na nafasi ya pekee katika moyo wa kiongozi wetu shahidi—Allah anyanyue daraja yake—na moja ya dalili zake ilikuwa ni maumivu katika sauti yake wakati wa hotuba ya swala ya Eid, alipoguswa na maafa ya mafuriko yaliyokuwa yakitishia maisha ya Waislamu wenzetu huko. Mimi mwenyewe pia, kwa sababu mbalimbali, siku zote nilikuwa na mtazamo kama huo, na sikuwa nikisita kuelezea hisia hizo katika vikao mbalimbali.
Hapa, ningependa kuwasilisha ombi kwamba nchi zetu mbili ndugu, Afghanistan na Pakistan, kwa ajili ya radhi ya Mwenyezi Mungu na ili kulinda umoja wa Umma wa Kiislamu, zifanye jitihada za kuimarisha uhusiano wao. Na kwa upande wangu, niko tayari kuchukua hatua zinazohitajika katika mipaka ya jukumu langu.
Na pia nakumbusha kwamba mashambulizi yaliyotokea nchini Uturuki na Oman, ambazo zote mbili zina mahusiano mazuri nasi, dhidi ya baadhi ya maeneo ndani ya nchi hizo, hayakufanywa kabisa na vikosi vya kijeshi vya Jamhuri ya Kiislamu au na nguvu nyingine zozote za upande wa muqawama. Hii ni hila inayotumiwa na adui wa Kizayuni kupitia mbinu ya “bendera ya uongo”, kwa lengo la kuleta mifarakano kati ya Jamhuri ya Kiislamu na majirani zake. Na inawezekana tukio kama hili kutokea pia katika nchi nyingine.
Mengine yanayohusiana na sehemu hii tayari niliyataja hapo kabla.
Natumai kwa dua za bwana wetu, Allah aharakishe kudhihiri kwake, na kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, mwaka ulio mbele yetu uwe mwaka mwema uliojaa ushindi na aina mbalimbali za faraja na mafanikio ya kimaada na kiroho kwa taifa letu, kwa majirani zetu wote, kwa mataifa ya Kiislamu, na hasa kwa wale waliomo katika safu za muqawama. Na uwe mwaka usio hivyo kwa maadui wa Uislamu na wa ubinadamu.
“Na tunataka kuwafadhilisha wale waliodhoofishwa katika ardhi, na kuwafanya kuwa viongozi, na kuwafanya kuwa warithi. Na kuwapa nguvu na mamlaka katika ardhi, na kumuonyesha Firauni na Haman pamoja na majeshi yao kupitia wao yale ambayo walikuwa wakiyahofia.” (Qur’ani)
Mwenyezi Mungu Aliyetukuka amesema kweli, na Mtume wake mtukufu amesema kweli, nasi juu ya hilo ni miongoni mwa mashahidi.
Na amani iwe juu yenu, na rehema za Mwenyezi Mungu, na baraka zake.
Sayyid Mujtaba Hosseini Khamenei
29 Esfand 1404 Hijria Shamsia
20 Machi 2026
3496836