IQNA

Hamas yatoa wito wa kulindwa Masjidul Aqsa

11:44 - April 14, 2014
Habari ID: 1395102
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imetoa wito kwa taifa la Palestina kuuhami na kuulinda Msikiti wa Al Aqsa.

Hii ni kufuatia tisho la Wazayuni wenye misimamo ya kufurutu ada ambao wametishia kuingia katika uwanja wa Msikiti wa Al Aqsa leo Jumatatu.  Imepangwa kuwa makundi hayo ya Wazayuni wenye misimamo mikali watauvamia Msikiti wa Al Aqsa chini ya himaya ya vikosi vya utawala haramu wa Israel.
Taarifa hiyo ya Hamas ambayo imetoa wito wa maandamano kote Palestina imeongeza kuwa, 'Kuna hatari kubwa katika hatua za uhasama utawala  wa Kizayuni ambao unauvunjia heshima Msikiti wa Al Aqsa'. Hamas imeuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel na makundi ya Wazayuni wenye misimamo mikali kuhusu hujuma yao dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa. Hamas imeongeza kuwa hujuma hiyo ya Wazayuni ni jinai kubwa na ni uvunjiwaji heshima Quds Tukufu.
Hamas katika taarifa hiyo imetoa wito wa wakuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kusitisha mazungumzo na utawala ghasibu wa Kizayuni kama njia ya kulalamikia hujuma dhidi ya Masjidul Aqsa.
Katika siku za hivi karibuni, vikosi vya utawala haramu wa Israel na walowezi wa Kizayuni wamekithirisha hujuma zao  dhidi ya Wapalestina katika Msikiti wa Al Aqsa. Aidha utawala wa Israel pia umekuwa ukiwazuia Wapalestina kuswali katika Msikiti wa Al Aqsa.
Kwa mfano siku ya Jumapili askari wa utawala wa Kizayuni waliwazuia Waislamu kupitia katika mlango mmoja wa Msikiti wa Al Aqsa. Hivi karibuni aidha Wapalestina walipambana na askari wa utawala wa Kizayuni wakati wa kuzinduliwa ramani ya hekalu moja la Kiyahudi katika uwanja wa Msikiti wa Al Aqsa. Duru zinaarifu Wazayuni wana mpango wa kujenga kile wanachokiita kuwa ni 'Hekalu la Tatau la Kiyahudi' katika eneo hilo. Ramani iliyozinduliwa inayonyesha kuwa hekalu hiyo inajumuisha ukumbi mkubwa wenye uwezo wa kubeba mamia ya watu. Kwa mujibu wa Shirika la Auqaf na Turathi za Utamadini Al Aqsa, mpango wa hekalu hiyo ni tishio kubwa na la moja kwa moja kwa Msikiti wa Al Aqsa. Shirika hilo limesema mradi huo wa hekalu umezinduliwa kwa lengo la kupata uungaji mkono wa Mayahudi katika kufadhili ujenzi wa hekali la Kiyahudi ndani ya uwanaja wa Msikiti wa Al Aqsa. Kwingineko Wapalestina pia wameonya kuhusu uchimbuaji mkubwa unaofanya na Israel karibu na mlango wa kusini wa kuingia Msikiti wa Al Aqsa. Bunge la Utawala wa Israel, Knesset, mnamo tarehe 25 Februari mwaka huu lilijadili kadhia ya kunyakua Msikiti wa Al Aqsa na kuufanya kuwa sehemu ya ardhi ambazo Israel ilizikali kwa mabavu mwaka 1948.
Shirika la Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu OIC imelaani vikali mjjadala huo ambao imeutaja kuwa wenye lengo la 'kuuiyahudisha Quds Tukufu'. Wapalestina pia wameonya kuhusu njama hiyo ya Israel ya kutekeleza kile inachokitaja kuwa ni 'haki ya mamlaka' katika Msikiti wa Al Aqsa.

1394785

captcha