Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Kikao hicho cha siku mbili kilichoanza jana kinahudhuriwa na zaidi ya wafanya biashara 100 maarufu kutoka nchi kama vile Tunisia, Misri, Syria, Lebanon, Bahrain, Imarati, Qatar, Saudi Arabia, Uturuki, Iraq, Jamhuri ya Azerbaijan, Tajikistan, Afghanistan na Urusi.
Kikao hicho kimeandaliwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu ya Kiislamu kwa lengo la kuarifisha fursa za kibiashara nchini Iran. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu Ayatullah Muhsin Araki ameelezea matumaini yake kuwa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara hatimaye utapelekea kupatikana umoja wa Kiislamu duniani. Amesema nguvu za kiuchumi ni nukta muhimi katika Uislamu kwani ni jambo litakalopelekea Waislamu kuwa na ushawishi duniani. Ayatullah Araki pia ameelezea udharura wa kuundwa banki ya kimataifa ya Kiislamu itayaoendesha shughuli zake kwa msingi wa sheria za Kiislamu. Mwanazuoni huyo mwandamizi amesema iwapo uhuriano wa kiuchumi utajengeka katika msingi wa taqwa, si tu kuwa umasikini utaondoka katika nchi za Kiislamu bali pia uadilifu utaenea kote dunianiani.Naye Mkuu wa Masuala ya Kijamii katika Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu Bw. Abdullah Sohrabi amesema kikao hicho kinatekeleza kivitendo ukuruba baina ya madhehebu ya Kiislamu kwa kuwaleta pamoja wafanya biashara kutoka nchi mbali mbali za Kiislamu.