IQNA

Imam Khamenei

Nchi za Kiislamu ziweke kando hitilafu zao ili ziisaidie Ghaza

19:57 - July 29, 2014
Habari ID: 1434650
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, 'ulimwengu wa Kiislamu kwa kuweka kando hilitalfu zilizopo, utumie uwezo wake wote kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.'

Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo Jumanne mjini Tehran katika kikao cha Baraza la Idul Fitr ambacho kimehudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu nchini, mabalozi na wawakilishi wa nchi za Kiislamu na wananchi wa matabaka mbali mbali. Katika hotuba yake Kiongozi Muadhamu pia ametoa wito kwa Ulimwengu wa Kiislamu kukabiliana kivitendo na jinai za Wazayuni sambamba na kutangaza kuchukizwa na kujibari kwao na waitifaki wa Wazayuni hasa Marekani na Uingereza. Sambamba na kutoa salamu zake kwa mnasaba wa siku kuu ya Idul Fitr kwa mataifa ya Waislamu, Ayatullah Khamenei amesema Idi hii ni Idi ya umma ulioungana. Ameongeza kuwa, ni jambo la kusikitisha kwamba kinyume na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu, leo tunaona mifarakano katika umma wa Kiislamu kutokana na sababu za kisiasa na tamaa ya madaraka. Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei ametoa wito kwa viongozi wa nchi za Kiislamu waondoe vizingiti hivyo vinavyozuia kuunda umma moja wa Kiislamu wenye nguvu na uwezo. Ameendelea kusema kuwa iwapo wenye tamaa ya madaraka, vibaraka na mafisadi hawataweza kuutenganisha umma wa Kiislamu, basi hakuna dola lolote lenye kiburi litakaloweza kuthubutu kuhujumu nchi za Kiislamu wala kuzishinikiza serikali za Kiislamu. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema ujuba wa Wazayuni katika kuwaua kwa umati Wapalestina Ghaza ni natija ya mifarakano katika Ulimwengu wa Kiislamu. Amesema kuwa, hatua ya vyombo vya habari vya magharibi kuficha ukweli ni jambo ambalo limepelekea watu wa nchi za Magharibi kutofahamu kina cha matukio ya Ghaza. Amesema jinai zinazotekelezwa Ghaza ni za kinyama na kuogofya kiasi kwamba hata habari chache zinazoakisiwa katika vyombo vya habari vya kimagharibi zimewashtua wasio kuwa Waislamu na kuwafanya wajitokeza mitaani kulaani jinai hizo. Kiongozi Muadhamu ameashiria masaibu na matatizo sugu ya watu wa Ghaza na kusema wanahitajia misaada ya dharura kama vile vyakula, dawa, maji, suhula za hospitali na ukarabati wa nyumba zao zilizoharibiwa. Ameongeza kuwa Wapalestina huko Ghaza pia wanahitajia silaha ili waweze kujilinda. Ayatullahil Udhma Khamenei ameendelea kusema kuwa uungaji mkono wa madola yenye kiburi hasa Marekani na Uingereza na pia uungaji mkono usio wa moja kwa moja au wa moja kwa moja wa taasisi za kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa kwa jinai za utawala wa Kizayuni ni jambo linalozifanya nchi na taasisi hizo kuwa washirika wa jinai za utawala huo katili ufyonzao damu.

Rais Rouhani: Iran inataka amani na uadilifu duniani, umoja wa Kiislamu


Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema stratijia ya Jamhuri ya Kiislamu ni kufuatilia amani na uadilifu  duniani, na katika ulimwengu wa Kiislamu ni kufuatilia umoja.
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo Jumanne mjini Tehran katika mkutano wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na maafisa wa ngazi za juu nchini, mabalozi na wawakilishi wa nchi za Kiislamu na wananchi wa matabaka mbali mbali kwa mnasaba wa Siku  Kuu ya  Idul Fitr.
Akihutubu katika baraza hilo la Idul Fitr, Rais Rouhani ameongeza kuwa, katika Ulimwengu wa Kiislamu, Iran inataka kuona udugu, umoja, mshikamano na juhudi za kuunda umma moja wa Kiislamu. Rais wa Iran amebainisha masikitiko yake kuwa, katika eneo na katika Ulimwengu wa Kiislamu kuna vivimbe viwili sugu vya saratani; amesema cha uvimbe wa kwanza ni ule ambao umewapelekea Wapalestina na Waislamu wapate uchungu mkubwa  na katika siku za hivi karibuni umepelekea umwagikaji mkubwa wa damu ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza. Rais Rouhani ameendelea kusema kuwa uvimbe wa pili sugu wa saratani  ni ule ambao umepelekea Waislamu wapate masaibu katika siku za hivi karibuni kupitia ile harakati ambayo imeanza kwa jina la Uislamu, dini, ukhalifa na imarati na kuanza kuwaua Waislamu na wasio kuwa Waislamu katika eneo. Amesema tathmini zinaonyesha wazi kuwa vivimbe hivi viwili vya saratani vinatoka sehemu moja. Rais Rouhani amesema njia pekee ya  kutatua matatizo hayo ni umoja wa nchi za Kiislamu. Amesema nchi za Kiislamu duniani zinapaswa kuwa zenye kutoa wito wa amani na uadilifu duniani huku zikiwasilisha muongozo wa kujiweka mbali na ujahili au ujinga na taasubu. Rais Rouhani pia ametoa wito wa kuandaliwa mazingira ya kufikishwa katika vyombo vya sheria watenda jinai katika utawala wa Kizayuni wa Israel.

1434614

 

captcha