Katika taarifa yake, Sheikh Shaaban ameitaja hatua hiyo ya Wazayuni kuwa aina mbaya zaidi ya hujuma zisizo na kikamo za Wazayuni dhidi ya Masjidul Aqsa.
Aidha mwanazuoni huyo wa Lebanon ametoa wito kwa wapenda uhuru kote duniani wachukue hatua za kuzuia jinai za utawala wa Kizayuni na kuunusuru Msikiti wa Al Aqsa.
Wakati huo huo hatua ya kiburi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ya kuuvunjia heshima msikiti wa al-Aqsa, imeibua hasira za Waislamu kote ulimwenguni. Nchini Misri mamia ya Waislamu wamefanya maandamano mbele ya ubalozi wa utawala huo mjini Cairo na kuichoma moto bendera ya utawala huo ghasibu. Aidha waandamanaji wamelaani ushirikiano uliopo baina ya Abdel Fattah el-Sisi, Rais wa hivi sasa wa Misri na utawala haramu wa Kizayuni unaoyavunjia heshima matukufu ya Waislamu na Wakristo duniani. Mjini Amman Jordan, maelfu ya Waislamu wamefanya maandamano makubwa kupinga hatua ya utawala huo, ya kufunga milango ya msikiti wa al-Aqsa na kuitaja hatua hiyo kuwa ni kucheza na hisia za Waislamu. Waandamanaji hao pia wametaka kukomeshwa mahusiano yoyote baina ya viongozi wa Amman na Tel Aviv. Itakumbukwa kuwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1967 utawala huo ghasibu ulifunga milango ya msikiti huo kwa siku mbili na kuifungua alfajiri ya jana Ijumaa kwa kuwaruhusu watu wenye umri wa miaka 50 na kuendelea kusali msikitini hapo. Kwa upande wake Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hii, Bi Marziye Afkham, imelaani vikali kitendo cha utawala huo wa Kizayuni kuuvunjia heshima msikiti huo wa al-Aqsa.../mh