Hapo jana askari wa Israel walikabiliana vikali na Wapalestina walikuwa wakiandamana kupinga hatua ya kufungwa eneo hilo tukufu la Waislamu katika maeneo tofauti ya Quds Mashariki na Ukingo wa Magharibi.
Wakati huo huo Muungano wa kimataifa wa taasisi zisizo za kiserikali zinazounga mkono wananchi wa Palestina umesema kuwa ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu na sheria za kimataifa unaofanywa na Wazayuni unapaswa kufuatiliwa kimataifa. Muungano huo pia umelaani jinai za Israel katika mji wa Baitul Muqaddas na kusema kuwa utawala huo bandia unapaswa kushtakiwa kimataifa kwa kuwakamata, kuwaua, kuwatesa vijana, wanawake na watoto kwa madai yasiyo na msingi ambayo ni kinyume na sheria za kimataifa.
Wakati huo huo Naibu Mkuu wa Idara ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ameutaka Ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu kuitetea na kuilinda Quds na Msikiti wa Alqsa mbele ya harakati na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Ismail Hania alitoa wito huo baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kufunga Msikiti mtakatifu wa al Aqsa Alkhamisi ilioyopita kwa kisingizio cha kushambuliwa kuhani mmoja wa Kiyahudi mwenye misimamo mikali. Kuhani wa Kizayuni mwenye misimamo ya kuchupa mipaka Yehudah Glick alipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya. Kuhani huyo ni miongoni mwa Wazayuni hatari sana na wahamasishaji wakubwa wa mashambulizi na hujuma dhidi ya Msikiti wa al Aqsa ambacho ni kibla cha kwanza cha Waislamu na vilevile mhamasishaji mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina.
Ismail Hania amesema katika mkutano wa kimataifa uliopewa jina la Mustakbali wa Mgogoro wa Uzayuni na Uislamu huko Palestina uliofanyika Gaza kwamba, hata kurejea katika Umoja wa Mataifa kwa ajili ya yale yanayoendelea huko Quds Tukufu hakutoshi na kuna ulazima wa kubuniwa mpango wa Kiislamu na Kiarabu katika misingi ya muqawama na mapambano.
Waziri mkuu wa zamani wa Palestina amesema kuwa ardhi ya Palestina na Quds ni mali ya Wapalestina na Waislamu na kwamba kuwahami na kuwaunga mkono Wapalestina wanaolinda na kutetea Msikiti wa al Aqsa na kuwadhaminia mahitaji yao ya kifedha na kisiasa kunapaswa kuwekwa katika mpango huo wa Kiarabu na Kiislamu.
Talal Nassar ambaye pia ni kiongozi mwandaminizi wa Hamas amesisitiza kuwa harakati hiyo haitanyamazia kimya jinai za Wazayuni maghasibu dhidi ya Msikiti wa al Aqsa na kuongeza kuwa, iwapo adui mzayuni atahujumu au kuvunjia heshima Msikiti huo Hamas itashambulia kwa makombora vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.
Jumapili iliyopita pia Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas alitoa raarifa akiashiria harakati za Wazayuni dhidi ya Msikiti wa al Aqsa na kutangaza kuwa, taifa la Palestina kamwe halitafumbia jcho hujuma na uvamizi wowote dhidi ya Msikiti wa al Aqsa.
Wakati huo huo Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imetoa taarifa mwishoni mwa kikao chake cha dharura mjini Cairo ikilitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupasisha azimio la kukomeshwa uvamizi wa Israel dhidi ya Palestina.
Misimamo hiyo ya kupinga njama za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Msikiti wa al Aqsa imekuja wakati Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akidai kuwa habari ya kufungwa Msikiti wa al Aqsa ni ya uongo.
Baada tu ya madai hayo Naibu Spika wa Bunge la Israel Moshe Feiglin alivamia Msikiti wa al Aqsa akiwa pamoja na wabunge wenzake kadhaa wenye misimamo ya kufurutu ada na walowezi wa Kiyahudi wakisindikizwa na jeshi la Israel. Hatua hiyo ilikabiliwa na makumi ya Waislamu wa Kipalestina waliokuwa katika eneo la Msikiti wa al Aqsa waliopiga takbira na kukabiliana na Wazayuni hao. Mapambano hayo yalimlazimisha Moshe Feiglin na wenzake kuondoka katika msikiti huo mtakatifu.../mh