IQNA

Waislamu Uganda, Ethiopia washerehekea Maulid ya Mtume SAW

16:17 - January 06, 2015
Habari ID: 2677812
Tehran-IQNA- Waislamu nchini Uganda Jumamosi iliyopita waliadhimisha Maulid (kumbukumbu ya kuzaliwa ) Bwana Mtume Muhammad SAW huku wakitoa wito wa amani na umoja katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki inayokumbwa na migawanyiko miongoni mwa Waislamu.

“Tunaweza kuufahamu Uislamu kwa njia bora zaidi iwapo tu tutaungana,” amesema Mufti Mkuu wa Uganda Sheikh Zubair Kayongo,
“Tukiendelea kuhubiri kuhusu mauaji, utumiaji mabavu na kuwapokonya wengine mali zao, ni vipi Uislamu utaenea ana kustawi katika nchi hii?”
Sherehe hizo za Miladun Nabii zinafanyika nchini Uganda huku Waislamu wakisubiri matokeo ya uchunguzi wa polisi kuhusu mauaji ya Mashekhe Waislamu mwezi uliopita wa Desemba.
Ikumbukwe kuwa kiongozi mwandamizi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Uganda Sheikh Ductoor Abdul Qadir Sudi Muwaya aliuawa shahidi.
Shahidi Sheikh Abdul Qadir ambaye alikuwa muasisi na mkurugenzi wa Taasisi ya Kiislamu ya Ahlul Bait  AS alipigwa risasi na watu wasiojulikana mbele ya nyumba yake muda mfupi tu baada ya kuswali sala ya Ishaa na kusoma  Dua Kumayl katika msikiti wa Buyemba.
Siku chache baadaye Sheikh Mustafa Bahiiga wa kundi la Tablig naye pia aliuawa katika eneo la Kampala na watu wasiojulikana.
Polisi nchini Uganda wamedai kuwa wasomi hao Waislamu waliuawa na waasi wa kundi la ADF ambalo lina misimamo mikali na lenye makao yake katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mufi wa Uganda Sheikh Ramadhan Mubajje naye pia ametoa wito wa umoja miongoni mwa Waislamu Uganda. Akiwahutubia Waislamu katika Msikiti wa Kibuli mjini Kampala, Sheikh Mubajje amesema umoja ndio utakaowezesha Waislamu kusonga mbele.
Nchini Ethiopia pia Waislamu walikusanyika katika Msikiti Mkuu wa Anwar katika mji mkuu wa nchi hiyo Addis Ababa kusherehekea Maulid ya Mtume Muhammad SAW. Maelfu ya Waislamu walikusanyika katika msikiti huo mkongwe katika sherehe ambazo zlilihudhuriwa na viongozi wa Kiislamu kutoka kote Ethiopia.  Akizungumza katika hafla hiyo Naibu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Maswali ya Kiislamu Ethiopia Sheikh Kedir Mohamoud Aman ametoa wito kwa Waislamu kujihusisha katika siasa kwa kupiga kura ili viongozi wanaostahiki waweze kuchaguliwa.

2672093

captcha