Akihutubu kabla ya sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo mjini Tehran, Ayatullah Muhsin Araki amebainisha njama za maadui wa umma wa Kiislamu za kuzusha fitina na mifarakano baina ya Waislamu na kusisitiza kwamba, maadui wanaelewa wazi kwamba, iwapo Waislamu watashikamana na kuwa kitu kimoja, kuna uwezekano wa kuwa na nguvu kubwa zaidi ulimwengu katika siku zijazo. Ayatullah Araki ameongeza kuwa, maadui kwa kutumia Ushia na Usuni wanachochea hitilafu na mifarakano katika nchi za Iraq, Syria, Yemen na katika maeneo mengine ya ulimwengu wa Kiislamu ili waweze kuzuia kuundwa umma mmoja wa Kiislamu wenye nguvu kubwa duniani. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu ya Kiislamu ameelezea baadhi ya hitilafu za kimitazamo zilizoko baina ya Masuni na Mashia na kusisitiza kuwa, makundi hayo yote mawili ni ya Kiislamu na yanaamini kuwepo Mwenyezi Mungu mmoja, utume wa Nabii Muhammad (saw), Qurani Tukufu na Kibla kimoja. Ayatullah Araki ameongeza kuwa, uadui na chuki kubwa za serikali za Marekani, Uingereza na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zinatokana na misaada na uungaji mkono wa taifa la Iran kwa wananchi madhulumu wa Palestina.../mh