Imearifiwa kuwa hujuma hiyo ya kinyama imefanyika wakati Waislamu walipokuwa wakitekeleza Swala ya Ijumaa katika msikiti huo ulio katika wilaya ya Sawabir katika mji mkuu wa Kuwait. Kundi la kigaidi na Kitakfiri la Daesh (ISIS) limedai kuhusika na hujuma hiyo.
Emir wa Kuwait Sheikh Sabah al-Ahmad al-Jaber al-Sabah ametembelea eneo la hujuma hiyo na kulaani kitendo hicho cha ugaidi. Baraza la Mawaziri Kuwait limeitisha kikao cha dharura huku Wizara ya Mambo ya Ndani nchini humo ikianzisha uchunguzi sambamba na kuimarisha usalama.
Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amelaani hujuma hiyo ya kigaidi. Katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Kuwait, Sabah Al-Khalid al-Hamad al-Sabah, Zarif amesema kuna haja ya kuwepo ushirikiano wa nchi zote ili kuangamiza kikamilifu ugaidi. Naye msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bi. Marzieh Afkham amelaani vikali hujuma hiyo ya kigaidi dhidi ya mskiti nchini Kuwait. Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeshatangaza mara kadhaa kuwa ugaidi wa Kitakfiri ni tishio kwa eneo zima na kwamba kuna haja ya kuwepo ushirikiano wa kieneo kukabiliana na tishio hilo na kuliangamiza.
Katika wiki za hivi karibuni magaidi wa Daesh wametekeleza hujuma dhidi ya misikiti ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Saudi Arabia na Yemen ambapo makumi ya watu wakiwemo watoto, wameuawa.../mh