IQNA

Maulamaa Waislamu Ghana

Vijana waisome Qur'ani ili wasitumbukie mtego wa ISIS

16:18 - September 08, 2015
Habari ID: 3360612
Maulamaa wa Kiislamu nchini Ghana wametangaza msimamo wa kupinga vikali kundi la kigaidi la Daesh au ISIS na kutoa wito kwa vijana nchini humo kuisoma na kufahamu ipasavyo tafsiri ya Qur'ani kwa njia sahihi ili wasitumbukie katika mtego muovu wa ISIS.

Katika taarifa yao hivi karibuni, Maulamaa wa Kiislamu Ghana wametangaza bayana kuwa harakati za makundi ya kigaidi ni kinyume cha mafundisho ya Kiislamu na hivyo wamewataka vijana kuchukua tahadhari ili wasiingie katika makundi yenye misimamo mikali kama vile Boko Haram na ISIS.
Tahadhari hiyo imetolewa na Maulamaa wa Ghana baada ya vijana kadhaa wa Ghana kujiunga na makundi ya kigaidi. Katika taarifa yao, viongozi hao wa Kiislamu wamesema ISIS na makundi mengine yanayodai kuwa ya Kiislamu ni bandia na kwamba yana ufahamu usio sahahi hata kidogo wa Uislamu na ndio sababu ya wao kuwaua watu wasio na hatia kwa malengo yao ya kisiasa, kiaidiolojia na kiuchumi.
Sheikh Armiyawo Shaibu mjumbe wa Baraza la Ushauri la Maimamu Waislamu Ghana na Sheikh Salman Mohammed Alhassan Mwenyekiti  Taifa wa Jumuiya ya Ahlul Sunna wal Jamaat nchini Ghana katika mahojiano tafauti na gazeti la Daily Telegraph la nchi hiyo wamesisitiza kuwa kile ambacho kinafanywa na makundi ya kigaidi yenye misimamo mikali hakina uhusiano wowote na Uislamu.
Aidha wamesema ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya Waislamu wenye ufahamu duni wa Uislamu wameshawishiwa na makundi ya kigaidi kupitia mitandao intaneti na kujiunga na makundi hayo yanayowaua  watu wasio na hatia.
Hivi karibuni kijana Mwislamu Ghana Nazir Nortei Alema alijiunga na kundi la kigaidi la ISIS nchini Syria. Alema ambaye ana shahada ya chuo kikuu katika taalamu ya jiografia na maendeleo vijijini ni miongoni mwa vijana 10 Waislamu nchini Ghana ambao wamejiunga na ISIS.
Akiashiria kujiunga kijana huyo na ISIS, Sheikh Armiyawo Shaibu  amesema Waislamu nchini Ghana wameshtushwa sana na kijana kama Nazir Alema kujiunga na ISIS. Amesisitiza kuwa Uislamu ni dini ya amani na maelewano  na kwa hivyo idiolojia ya ISIS inapinga kabisa na mafundisho ya Qur'ani na sira ya Mtume Muhammad SAW.
Naye Sheikh Salman Mohammed ametoa wito kwa vijana Waislamu kutohadaiwa na Maulamaa bandia walio katika mitandao ya kijamii kwani wanaeneza Uislamu ghalati.. Aidha amewataka vijana kuwasiliana na maulamaa wenye uelewa sahihi wa tafsiri sahihi ya Qur'ani Tukufu na Sunna ya Mtume SAW ili wasitumbukie katika mtengo wa ISIS.../mh

3360081

captcha