IQNA

Uvamizi wa Wazayuni katika msikiti wa al-Aqsa wasababisha umwagaji damu

13:35 - September 14, 2015
Habari ID: 3362433
Jumapili ya jana msikiti mtakatifu wa al-Aqsa kwa mara nyingine tena ulivamiwa na Wazayuni waliojumuisha wanajeshi, polisi na Wazayuni wenye misimamo ya kufurutu ada ambapo damu za makumi ya Wapalestina zilimwagwa kiholela katika tukio hilo.

Ripoti zinaonesha kuwa, zaidi ya Wapalestina 100 waliokuwamo msikitini hapo kwa ajili ya kutekekeza ibada ya Swala wamejeruhiwa. Sambamba na uvamizi huo mkubwa wa Wazayuni dhidi ya msikiti wa al-Aqsa, Waziri wa Kilimo wa utawala wa Kizayuni wa Israel Uri Ariel akiwa pamoja na kundi la Wazayuni wenye misimamo mikali aliingia katika uwanja wa msikiti huo, hatua inayotathminiwa na wajuzi wa mambo kwamba, ni ya kichochezi. Kwa hakika hatua hiyo inaonesha kubobea utawala wa Kizayuni wa Israel katika kutekeleza mipango iliyoratibiwa ya kuyavunjia heshima maeneo matakatifu. Njama za Wazayuni za kutaka kuubadilisha msikiti wa al-Aqswa ambao ni moja ya maeneo matakatifu ya wafuasi wa dini za Mwenyezi Mungu hususan Waislamu zimeligeuza eneo hilo na kuwa uwanja wa vita, jambo ambalo kwa mara nyingine tena limeweka wazi sura na utambulisho halisi wa Israel ulio dhidi ya dini, utawala ambao katu haufungamani na sheria za kimataifa. Hujuma na uvamizi mkubwa wa utawala wa Kizayuni dhidi ya msikiti wa al-Aqsa umekabiliwa na radiamali ya makundi mbalimbali ya Palestina. Kuhusiana na hilo, Izzat al-Risheq, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kuwa, kuingia Uri Ariel Waziri wa Kilimo wa Israel na walowezi wa Kiyahudi wenye kufurutu mpaka katika msikiti wa al-Aqsa kwa himaya ya jeshi la Israel bila shaka ni jinai ya kivita ambayo lengo lake ni kuupatia nguvu mpango mchafu wa kuugawa msikiti huo mtakatifu. Afisa huyo wa Hamas ameongeza kuwa, unyama na jinai za Israel dhidi ya msikiti mtakatifu wa al-Aqsa ni hatua hatari ambayo inafanyika katika fremu ya jinai mtawalia za adui Mzayuni dhidi ya msikiti huo na matukufu ya Kiislamu huko Quds. Tangu utawala wa Kizayuni utangaze uwepo na kuasisiwa kwake, Baytul Muqaddas na Masjid al-Aqsa vimegeuzwa na kuwa kitovu cha siasa za satwa na hatua za uharibifu za utawala huo vamizi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina. Moja ya hujuma kubwa za uharibifu za Israel dhidi ya msikiti wa al-Aqsa ni ile ya Agosti 1969 ambapo Mzayuni mwenye misimamo mikali aliyejulikana kwa jina la Michael Rohan aliuchoma moto msikiti huo kwa uratibu na viongozi wa Israel ambapo tukio hilo lilipelekea sehemu ya msikiti kuharibiwa. Kama vile haitoshi, Aprili 11 mwaka 1982 mwanajeshi mmoja wa Israel aliuvamia msikiti wa al-Aqsa na kuwamiminia risasi waumini wa Kipalestina waliokuwa wakiswali ambapo makumi kati yao waliuawa shahidi na kujeruhiwa. Kwa hakika utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukitekeleza hatua mbalimbali za kutaka kuuharibu msikiti wa al-Aqsa. Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, Baytul Muqaddas na Msikiti wa al-Aqsa sasa vinakabiliwa na duru mpya ya vitisho na njama za utawala wa Kizayuni wa Israel ambapo moja ya njama hizo ni mpango mchafu wa utawala huo ghasibu wa kutaka kuugawa msikiti huo katika sehemu mbili za Wapalestina na Wazayuni na kugawa pia nyakati za kuingia na kutoka katika msikiti huo. Katika mazingira kama haya ya njama mtawalia za Wazayuni maghasibu dhidi ya msikiti wa al-Aqsa, bila shaka kuna udharura kwa Wapalestina, Waislamu na jamii ya kimataifa kuonyesha radimali zao za kukabiliana na njama hizo za Wazayuni za kila siku iendayo kwa Mungu.../mh

3362236

captcha