Hafla hiyo ilihudhuriwa na maulamaa, maaisa wa kisiasa na kiutamaduni akiwemo Mkuu wa Shirika la Awqaf la Iran Hujjatul Islam Ali Mohammad na Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Kermanshah Ayatullah Ulama na Mkuu wa Mrengo wa Qur’ani katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, Bil Laleh Eftikhari.
Kikao hicho kilianza kwa qiraa ya Qur’ani Tukufu ambapo msomi alikuwa qarii mashuhuri Vahid Nazarian na kufuatiwa na ripoti fupi ya mashindano hayo iliyowasilishwa na Hujjatul Islam Husseini Araki mkuu wa Idara ya Awqaf mkoani Kermanshah. Aliyataja mashindano hayo ya wiki moja kuwa ni baraka kubwa kwa wakaazi wa eneo hilo. Aidha katika hafla hiyo kumezinduliwa baadhi ya vitabu vilivyoandikwa kuhusu Qur’ani Tukufu huku maustadhi wakongwe wa Qur’ani nchini Iran nao wakitunukiwa zawadi.
Halikadhalika walioshika nafasi za juu katika mashindano hayo wametunukiwa zawadi. Mashindano hayo yalikuwa na washiriki zaidi ya 630 wakiwemo maqarii na waliohifadhi Qur’ani kutoka maeneo yote ya Iran.
Mashindano ya kitaifa ya Qur’ani Iran hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuvumbua vipaji vya Qur’ani miongoni mwa washiriki na vilevile kuimarisha na kustawisha utamaduni na harakati za Qur’ani nchini.