IQNA

Uingereza yatisha kuwatimua wanawake Waislamu

13:18 - January 19, 2016
Habari ID: 3470064
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron ametisha kuwatimuwa wanawake wahamiaji Waislamu nchini humo iwapo hawatajifunza lugha ya Kiingereza.

Cameron amewataka wanawake hao Waislamu kujifunza Kiingereza kwa kiwango cha juu kinachotakiwa, la sivyo watatimuliwa nchini humo. Waziri Mkuu wa Uingereza amedai kuwa eti watu wasio na ufahamu sahihi wa lugha ya Kiingereza wanaweza kutumbukia katika ushawishi na kupotoshwa na jumbe za propaganda za makundi ya kigaidi kama vile ISIS au Daesh.

Matamshi ya Cameron imekuja muda mfupi baada ya chama chake cha Kihafidhina au Conservative kuzindua mfuko wa kuwasaidia wanawake walioko katika jamii zilizotengwa kujifunza Kiingereza. Mfuko huo wenye kiasi cha dola milioni 28.5 za Marekani unapania kuzisaidia jamii za Waingereza kutangamana. Hata hivyo kauli ya Waziri Mkuu wa Uingereza imekosolewa vikali na asasi za kiraia, upinzani na mashirika ya Kiislamu nchini humo. Muhammed Shafiq, Mkurugenzi Mkuu wa Wakfu wa Ramadhan (Ramadhan Foundation) amesema, kwa mara nyingine serikali ya nchi hiyo inatumia jina la Waislamu na Uislamu kujitafutia umaarufu wa kisiasa.

Naye mwenyekiti mwenza wa zamani wa chama cha Kihafhidhina Sayyeeda Warsi amesema mtazamo wa Cameroon ni ishara ya kuwa na fikra potovu na pia ni kuwabagua Waislamu Uingereza. Takwimu za serikali ya UK zimeonyesha kuwa, kati ya wanawake Waislamu laki moja na elfu 90 wanaoishi nchini humo, asilimia 22 hawana ufahamu kabisa au wana ufahamu mdogo wa lugha ya Kiingereza.

Kuna takriban Waislamu milioni 2.7 kati ya idadi ya watu milioni 53 nchini Uingereza.

3468607

captcha