Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, baadhi ya Waislamu katika nchi za Kiarabu na maeneo mengine duniani wameanza saumu kwa kutegemea tangazo lililotolewa na Saudi Arabia kuhusu kuanza mwezi Mtukufu wa Ramadhani hii leo. Nchi kama vile Yemen, Kuwait, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu, Jordan na Qatar zimetangaza leo kuwa siku ya kwanza ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Kwingineko, nchi za Kiislamu kama vile Oman, Jamhuri ya Kislamu ya Iran, Morocco na Brunei zimetangaza rasmi kuwa siku ya kwanza ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni Jumanne Juni 7 baada ya kuthibitika kuwa mwezi haujaandama. Aidha Kadhi Mkuu wa Kenya Sheikh Ahmad Muhdhar Jumapili jioni akizingumza mjini Mombasa alithibitisha kuwa mwezi haukuonekana nchini Kenya wala katika maeneo ya Afrika Mashariki na kwa msingi huo akatangaza kuwa Ramadhani itaanza siku ya Jumanne 7 Juni. Aidha Kadhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Tanzania Sheikh Hamid Masoud Jongo amenukuliwa akitoa tangazo kwa niaba ya Mufti wa Tanzania kuwa leo Juni 6 2016 ni sawa na 30 Shaaban 1437 Hijria kesho Jumanne itakuwa tarehe Mosi Ramadhani.