Watoto hao waliuawa siku ya Jumatatu wakati ndege za kivita za Saudia zilipodondosha mabomu ya vishada katika wilaya ya Sahari mkoani Sa’ada kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Hayo yanajiri wakati ambao Jamie McGoldrick, Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen amethibitisha kuwa vita vya miezi 18 nchini Yemen vimesababisha vifo vya watu wasiopungua elfu kumi.
Kabla ya hapo, licha ya duru za ndani ya Yemen kutangaza kuwa hujuma na mashambulio ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu yameua zaidi ya watu elfu kumi, maafisa wa Umoja wa Mataifa walikuwa wakisisitizakwamba idadi ya watu waliouawa ni zaidi ya elfu sita tu.
Hata hivyo katika mkutano aliofanya leo na waandishi katika mji mkuu wa Yemen Sana'a, Jamie McGoldrick ametangaza kuwa kulingana na takwimu za duru za tiba na hospitali nchini humo idadi ya watu waliofariki kutokana na mashambulio ya muungano vamizi unaoongozwa na utawala wa Aal Saud imefikia elfu kumi.
McGoldrick ameongeza kuwa kuna uwezekano idadi ya watu waliouawa katika vita vya Yemen ikawa kubwa zaidi ya hiyo kwa sababu kutokana nabaadhi ya maeneo kutokuwa navituo vya tiba, hakuna taarifa zilizorekodiwa kuhusu idadi ya vifo.
Aidha amefafanua kuwa katika maeneo mengine baada ya watu kuuawa, ndugu na jamaa zao huharakisha kuwazika pasina kutoa taarifa kwa vyombo husika.
Alkhamisi iliyopita, ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilitoa taarifa na kutangaza kuwa mashambulio ya anga ya muungano unaoongozwa na Saudia dhidi ya Yemen ndiyo sababu kuu ya vifo vya raia3,799 na kujeruhiwa wengine 6,711.
Kwa mujibu wa ofisi hiyo, mbali na mauaji, muungano vamizi unaoongozwa na Saudia umehusika pia na makosa mengine ambayo yanaweza yakawa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Itakumbukwa kuwa mapema mwezi Juni, Umoja wa Mataifa, kupitia ripoti ya Katibu Mkuu wake Ban Ki-moonuliiweka Saudi Arabia kwenyeorodha nyeusi ya nchi zinazokiuka haki za watoto kutokana na mauaji ya kutisha unayotekeleza dhidi ya mamia ya watoto wadogo wasio na hatia huko Yemen.
Hata hivyo Ban alibadilisha uamuzi wake huo baadaye baada ya utawala wa Aal Saud kutishia kukata misaada na ufadhili wake wakifedha kwa Umoja wa Mataifa.
Tangu ulipoanzisha uvamizi wake wa kijeshi dhidi ya Yemen mnamo mwezi Machi mwaka uliopita, hadi sasa muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa nautawala wa Aal Saud na kuungwa mkono na Marekani umesha zishambulia skuli, hospitali, maeneo ya makaazi ya raia, barabara, masoko na kambi za wakimbizi na kuua maelfu ya raia wasio na hatia wa nchi hiyo.