IQNA

Mahakama ya Rufaa Kenya yaruhusu vazi la Hijabu katika shule

12:57 - September 10, 2016
Habari ID: 3470557
Mahakama ya Rufaa nchini Kenya imeamuru wasichana Waislamu nchini humo wanaruhusiwe kuvaa vazi la stara ya mwanamke wa Kiislamu Hijabu wakiwa shuleni.

Uamuzi huo wa kihistoria uliotolewa na majaji watatu umekuja baada ya kanisa la kimethodist kupinga muongozo kutoka kwa mamlaka za nchi hiyo kuwaruhusu wasichana wa shule wa Kiislamu kuvaa hijab au vitambaa vya kichwa katika shule yake.

Wanafunzi wa Kiislamu katika shule ya sekondari ya St Paul Kiwanjani School Kaunti ya Isiolo walipigwa marufuku kuvaa Hijabu na suruali nyeupe pamoja na sare ya shule.

Kanisa hilo lilidai kuwa, uamuzi wa kuwaruhusu wanafunzi wasichana wa Kiislamu kuvaa mavazi tofauti umesababisha uhasama miongoni mwa wanafunzi wa shule hiyo.

Kwa upande wake mahakama ya juu nchini Kenya ilikuwa imeunga mkono msimamo wa kanisa na kusema kuwa wasichana hawawezi kuvaa hijabu wakiwa shuleni.

Hata hivyo majaji katika mahakama ya rufaa wamesema kuwa, ni jukumu la wanaotoa elimu kukubali maadili na kanuni za utu, na za matabaka mbali mbali ya watu na tena bila ubaguzi.

Duru za karibu na mahakama hiyo zinasema kuwa, majaji hao wamesema katika uamuzi wao huo kwamba, vazi la kidini haliwezi kulinganishwa na mtindo wa mavazi unaokwenda na wakati.

Wataalamu wa mambo wamesema kuwa, uamuzi huo wa Mahakama ya Rufaa wa kuruhusu wasichana wa Kiislamu kuvaa Hijabu shuleni ni ushindi wa jamii ya Waislamu nchini humo ambao walikuwa wamesononeshwa na hatua ya Mahakama ya Juu ya kuunga mkono uamuzi wa sekondari ya St Paul Kiwanjani School Kaunti ya Isiolo wa kuwapiga marufuku wasichana wa Kiislamu kuvaa Hijabu na suruali nyeupe pamoja na sare ya shule.

3529115
captcha