Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Bw. Mehdi Agha-Ja'afari, Balozi wa Iran nchini Tanzania ameyasema hayo Jumanne usiku mjini Dar es Salaam katika sherehe za kumuaga. Hafla hiyo iliandaliwa na Kamati ya Haki na Amani ya Viongozi wa Dini nchini Tanzania.
Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa kidini na kisiasa katika nchi hiyo akiwemo makamu wa zamani wa rais wa Tanzania Gharib Bilal, Sheikh Mussa Salim Al Hadi , Shehe mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Haki na Amani ya Viongozi wa Dini, viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania na mabalozi wa nchi za Kiislamu.
Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Agha-Ja'afari ameashiria nafasi ya Palestina na mji wa Quds (Jerusalem) miongoni mwa Waislamu na kusema: "Quds ni suala muhimu zaidi kwa Waislamu na wapigania uhuru kote duniani."
Ameongeza kuwa, 'Israel (inayokalia Quds kwa mabavu) ndio tatizo kubwa zaidi katika dunia na aghalabu ya matatizo na maafa katika eneo hutokana na kusahauliwa kadhia ya Palestina."
Balozi wa Iran nchini Tanzania anayeondoka amesema kunapaswa kufanyika vikao mbali mbali kuhusu Palestina na kuongeza kuwa, maadamu Wapalestina wamepokonywa haki zao, dunia haitashuhudia utulivu hata siku moja.
Mwishoni mwa hotuba yake, ameashiria jitihada za serikali ya Tanzania katika kuhakikisha Watanzania wote wanaishi kwa Amani na maelewano na kusema viongozi wa Tanzania wamefanikiwa katika kuleta mazingira hayo ya maelewano baina ya wafuasi wa dini mbali mbali.