IQNA

Mwenye chuki dhidi ya Uislamu ashindwa katika uchaguzi Uholanzi

16:24 - March 16, 2017
Habari ID: 3470898
IQNA:Matokeo ya uchaguzi wa bunge Uholanzi yanaonyesha mwanasiasa mwenye misimamo mikali na chuki dhidi ya Uislamu amepata pigo.
Kwa mujibu wa matokeo ya awali chama cha PVV ( Party for Freedom)  cha mwanasiasa mwenye misimamo mikali ya kibaguzi na chuki dhidi ya Uislamu, Geert Wilders , kimepata viti 20 huku chama cha VVD (Party for Freedom and Democracy) cha waziri mkuu wa sasa Mark Rutte kikiwa kimepata viti 33 katika Bunge la Uholanzi lenye viti 150. Pamoja na hayo chama chenye misimamo mikali kimepata viti vingi zaidi katika uchaguzi huu kwani hapo kabla kilikuwa na vitu 12 huku chama cha VVD cha waziri mkuu nacho kikionekana kupoteza umashuhuri kwani huko nyuma kilikuwa na viti 41.
Katika matokeo mengine Vyama vya Christian Democrats na Democrats vimepata viti 19 kila kimoja huku vyama vilivyosalia vya Kijani, Leba na Soshalisti vikinyakua viti vilivyosalia. Asilimia 81 ya wapiga kura wanaripotiwa kushiriki katika uchaguzi huo wa Jumatano na idadi hiyo imetajwa kuwa ya kihisotria.  
Mwezi Disemba mahakama moja ya Uholanzi ilimpata wilders na hatia  ya kuwatusi watu wenye asili ya Morocco na kuwabagua.

Kile kilichopelekea jina la Wilders kupata umashuhuri katika miaka ya hivi karibuni ni hatua yake ya kutengeneza filamu ya kuivunjia heshima Qur'an Tukufu ambacho ni kitabu cha mbinguni cha Waislamu, filamu iliyoitwa jina la 'Fitina.'

Utengenezwaji wa filamu hiyo uliibua malalamiko ya Waislamu duniani kote na hata kufunguliwa mashtaka dhidi ya mwanasiasa huyo katika mahkama za Uholanzi.

Kufuatia ushindi wa Donald Trump mwenye chuki dhidi ya Uislamu katika uchaguzi wa rais Marekani, wanasiasa wenye misimamo mikali ya mrengu wa kulia kote Ulaya nao pia wamepata matumaini ya kunyakua madaraka. Hatahivyo matokea ya uchaguzi wa Uholanzi yameonysha kuwa watu wa Ulaya hawataki wanasiasa wenye misimamo mikali ya kufurutu ada.

Kwa kushindwa wanasiasa wenye misimamo mikali Uholanzi, kuna matumaini pia kuwa wanasiasa wenye misimamo kama hiyo ya kufurutu ada nao pia watashindwa Ujerumani na Ufaransa, nchi ambazo zinatarajia kufanya chaguzi hivi karibuni.

3584709


captcha