
Ayatullah Sayyed  Ali Khamenei, Kiongozi wa Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu 
ameyasema hayo leo mjini Tehran kwa mnasaba wa sherehe ya siku ya kuzaliwa Bibi 
Fatima Zahraa SA binti wa Mtume Muhammad SAW alipokutana na wasomaji
 wa tungo za kumsifu Mtume na Ahlu Baiti wake AS. Amesisitizia pia umuhimu wa kuelewa nafasi chanya ya mwanamke wa Kiislamu. 
Kiongozi Muadhamu amesema kuna 
uwezekano mkubwa kwamba kumfanya mwanamke kuwa chombo cha anasa katika 
ulimwengu wa Magharibi, ni sehemu ya njama za Wazayuni kwa ajili ya 
kusambaratisha jamii ya mwanadamu.
Sambamba na kubainisha sababu ya kuenezwa nara za kama ile ya 'uadilifu 
na usawa wa kijinsia' katika nchi za Magharibi, amesema kuwa uadilifu ni
 kutambua vipawa na tunu alizopewa na Mwenyezi Mungu kuzistawisha.
Kiongozi Muadhamu amesema kuwa, hii leo wasomi wa Magharibi na watu 
wanaonadi usawa wa kijinsia wanajutia hatua yao hiyo kutokana na makosa 
mengi yanayosababishwa na suala hilo. Vilevile ameashiria sira na 
harakati adhimu ya Bibi Fatima Zahraa AS, mwanamke mtukufu wa Kiislamu
 katika nafasi ya kiongozi halisi na wakati huo huo kama mke na mama wa 
aina yake na kumtaja kuwa ni kiigizo chema na kamili kwa ajili ya 
Waislamu.' 
Itakumbukwa kuwa, siku kama ya leo miaka 1446 iliyopita yaani sawa na tarehe 20 Jamadu 
th-Thani mwaka wa nane kabla ya Hijiria, alizaliwa Bibi Fatima Zahraa 
SA Binti ya Mtukufu Mtume Muhammad SAW. Tangu utotoni mwake, Bibi 
Fatima alikulia katika nyumba ya wahyi na chini ya malezi bora ya baba
 yake Nabii wa Allah na hivyo kufikia daraja la juu la ukamilifu katika 
elimu na ubora. Aidha Bibi Fatimah SA alikuwa na nafasi muhimu katika
 kupunguza machungu na tabu zilizokuwa zikimkumba baba yake katika 
harakati za kueneza mafundisho ya dini ya Uislamu, kutoka kwa 
washirikina.
 Mwaka wa pili Hijiria binti huyo mtukufu wa Mtume alifunga 
ndoa kwa sherehe nyepesi sana na Imamu Ali Bin Abi Twalib, ambaye naye 
ni dhihirisho la haki, uadilifu na uchaji-Mungu. Akiwa na Imamu Ali SA  Bibi Fatimah aliishi kwa Amani na furaha ya juu huku akitekeleza 
majukumu ya mke na mama mwema kwa watoto wake watukufu, yaani Imamu 
Hassan AS, Imamu Hussein AS na Bibi Zainab SA.