IQNA

Mkutano wa kimataifa wa Uchumi wa Kiislamu/Halal wafanyika Kenya

18:04 - April 10, 2017
Habari ID: 3470929
TEHRAN (IQNA)-Mji mkuu wa Kenya, Nairobi leo ni mwenyeji wa mkutano wa siku mbili ambao unachunguza namna nchi hiyo inaweza kunufaika na uchumi wa Kiislamu au uchumi Halal ambao unashika kasi duniani.

Wataalamu wa kitaifa, kieneo na kimataifa katika sekta hiyo wanakutana mjini Nairobi katika mfremu ya Mkutano wa Kilele wa Afrika Mashariki wa Uchumi wa Kiislamu (EAIES) ambao unafanyika kwa mwaka wa pili.

Washiriki katika mkutano huo wanajadili fursa zinazopatikana katika biashara yenye thamani ya mabilioni ya dola ya bidhaa na huduma halali na namna Kenya na nchi zingine za Afrika Mashariki zinaweza kunufaika na biashara hiyo.

Uchumi 'Halal' umejengeka katika msingi wa mahitajio ya Waislamu zaidi ya bilioni 1.6 duniani ambao wanataka bidhaa na huduma ambazo zinaenda sambamba na mafundisho ya dini ya Kiislamu. Ili kuzalisha bidhaa au kutoa huduma halali si lazima mwenye kufanya hivyo awe Mwislamu.

Uchumi 'Halal' duniani unakadiriwa kuwa na thamani ya US$ Trilioni 2.3 na umetajwa kuwa sekta inayokuwa kwa kasi zaidi duniani.

Kongamano hilo pia linalenga kuondoa dhana potofu zilizopo kuhusu mfumo wa Kiislamu wa uchumi na fedha na kuangazia ubora wake.

Kenya hivi sasa iko katika mkakati wa kuigeuza nchi hiyo kuwa kitovu cha huduma za Kiislamu za kiuchumi na kifedha na tayari Wizara ya Fedha ya nchi hiyo iko katika mkakati wa kupitisha sheria na kanuni za kusimamia na kustawisha sekta hiyo.

Washiriki wa mkutano huo pia wanajadili fursa ambazo hazijatumiwa za uchumi 'Halal' Afrika Mashariki eneo ambalo lina mamilioni ya Waislamu wanaohitajia bidhaa na huduma kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu.

Kwa mfano Kenya ambayo ina vivutio vingi vya kitalii haijaweza kutoa huduma za kutosha za 'Utalii Halal' ambao soko lake duniani linakadiriwa kwa sasa kuwa na thamani ya US$ bilioni 219. Eneo la Zanzibar nchini Tanzania limefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutoa huduma za 'Halal' kwa watalii Waislamu.

/3588515
captcha