Hatua hiyo imekuja baada ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Bi.Jacinda Ardern kuamurisha kuwa Ijumaa ya leo adhana isomwe moja kwa moja kitaifa katika televisheni na radio sambamba na misikiti yote ya nchi hiyo. Aidha leo raia wa New Zealand wamenyamaza kimya kwa muda wa dakika mbili kama njia ya kutoa heshima yao kwa waliouawa katika hujuma misikitini. Halikadhalika misikiti yote ya nchi hiyo ilikuwa wazi Ijumaa kuanzia tangu asubuhi ili wasiokuwa Waislamu waweze kuitembelea na kujifunza kuhusu Uislamu.
Sala ya Ijumaa katika Bustani ya Hagley, Christchurch New Zealand
Halikadhalika Waziri Mkuu wa New Zealand amehudhuria Sala ya Ijumaa katika Bustani ya Hagley karibu na Msikiti wa al Noor akiwa amevalia Hijabu kama njia ya kuonyesha kufungamana na Waislamu nchini humo.
Wanaharakati katika mitandao ya kijamii nchini humo sambamba na kuanzisha kampeni ya vazi la hijab, wamewataka raia wa New Zealand kuzitembelea familia za wahanga wa shambulizi la kigaidi la Ijumaa iliyopita wakiwa wamevalia hijabu vichwani mwao.
Waziri Mkuu wa New Zealand Bi. Jacinde Adern akiwasili kujumuika na Waislamu katika Sala ya Ijumaa katika Bustani ya Hagley,Christchurch, New Zealand
Katika shambulizi la kigaidi la Ijumaa iliyopita katika misikiti ya Linwood na al-Noor mjini Christchurch, watu 52 waliuawa shahidi na wengine 47 kujeruhiwa. Aliyefanya unyama huo ni Brenton Tarrant, gaidi mwenye chuki na Uislamu mwenye uraia wa Australia. Gaidi Tarrant ni mfuasi sugu wa Rais Donald Trump wa Marekani ambaye ni mashuhuri kwa chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.
3799371