IQNA

12:36 - March 23, 2019
News ID: 3471886
TEHRAN (IQNA)- Kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kimefanyika Ijumaa mjini Istanbul, Uturuki kwa lengo la kujadili hatua za kuchukuliwa baada ya shambulio la kigaidi la hivi karibuni dhidi ya Waislamu waliokuwa katika Sala ya Ijumaa kwenye misikiti miwili nchini New Zealand.

Taarifa ya mwisho iliyotolewa baada ya kumalizika kikao hicho cha ngazi ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za OIC imesisitiza kuhusu kupambana kimataifa na uenezaji chuki dhidi ya Uislamu.

Taarifa hiyo iliyokuwa vipengele 20 imeeleza kuwa, jumuiya hiyo haikubaliani na mtazamo wa kuwatazama Waislamu kuwa ni watu wahalifu na kuwahusisha na ugaidi na vitendo vya kufurutu mpaka.

Sehemu moja ya taarifa hiyo ya OIC imeisifu na kuipongeza serikali ya New Zealand kwa kulaani mashambulio ya kigaidi pamoja na msimamo chanya ulioonyeshwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo kuhusiana na Waislamu na pia hatua ya wananchi wa matabaka yote ya jamii ya New Zealand ya kuwafariji Waislamu.

Sehemu nyingine ya taarifa ya kikao cha dharura cha OIC, mbali na kuipongeza serikali ya New Zealand kwa kukabiliana na njama za maadui, imezitaka pia nchi zenye jamii za Waislamu na jamii za kidini za wachache pamoja na watu wanaoomba hifadhi zijiepushe na siasa za kuuhusisha Uislamu na ugaidi.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu aidha imetoa mwito kwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Umoja wa Ulaya waasisi kituo cha haki za binadamu kitakachoripoti vitendo vya ukatili, chuki na uadui wa kidini.

OIC aidha imeutaka Umoja wa Mataifa na taasisi zingine za kimataifa ziitangaze Machi 15 kuwa Siku ya Mshikamano Duniani wa kukabiliana na uenezaji chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia).

Kikao hicho cha OIC mjini Istanbul kiliitishwa kufuatia pendekezo la Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif. Uturuki, kama mwenyekiti wa kiduru wa OIC, iliafiki pendekezo hilo la Iran na kwa msingi huo ikawa mwenyeji wa mkutano huo muhimu.

Itakumbukwa kuwa watu 52 waliuawa shahidi na wengine 47 walijeruhiwa katika shambulio la kigaidi la Ijumaa ya tarehe 15 Machi dhidi ya misikiti ya Linwood na Al-Noor mjini Cristchurch, New Zealand.

Aliyefanya unyama huo ni Brenton Tarrant, gaidi mwenye chuki na Uislamu mwenye uraia wa Australia. Gaidi Tarrant ni mfuasi sugu wa  Rais Donald Trump wa Marekani ambaye ni mashuhuri kwa chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.

3799418

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: