IQNA

Dunia yakumbuka kuuawa Shahidi Imam Hussein AS na wafuasi wake 72 huko Karbala

11:52 - September 10, 2019
Habari ID: 3472122
TEHRAN (IQNA) - Mamilioni ya Waislamu kote duniani hii leo wanaomboleza katika siku ya Ashura ambayo ni siku aliyouawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein AS.

Imam Husain AS aliuawa shahidi kikatili na kinyama mwaka wa 61 Hijria, yaani miaka 1380 iliyopita, katika jangwa la Karbala, Iraq ya leo, akiwa na umri wa miaka 57 baada ya kuongoza mapambano ya kishujaa ya ushindi wa damu mbele ya upanga.

Vita vya Karbala vilikuwa moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq. Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili ili kuilinda dini ya Allah. Hamasa ya Karbala ilikuwa dhihirisho la mambo mawili makuu. Kwanza ni ujasiri, ushujaa, moyo wa kujitolea, uaminifu pamoja na kuyapokea kwa moyo mkunjufu mauti ya kuuawa shahidi, sifa walizojipamba nazo wapiganaji wachache wa jeshi la haki wakiongozwa na Imam Hussein AS dhidi ya Yazid bin Muawiya. Pili ni upeo wa ukatili, udhalimu na unyama ulioonyeshwa na jeshi batili la Yazid bin Muawiya. Baada ya kupambana kishujaa, hatimaye mjukuu huyo wa Mtume Muhammad SAW aliuawa shahidi katika siku kama ya leo.

Mtume Muhammad SAW alitabiriwa na Malaika Jibril ukatili huo aliofanyiwa mjukuu wake katika jangwa la Karbala, tangu enzi za uhai wake na alikuwa wa kwanza kumlilia mjukuu wake huyo kipenzi baada ya kuletewa mchanga na Malaika Jibril, wa eneo ambalo Imam Hussein AS angeliuliwa shahidi.

Kwa kufuata sira na mwenendo huo wa Bwana Mtume Muhammad SAW, wafuasi wa Ahlul Bayt wa Mtume na wapenzi wa haki na wanaopiga vita dhulma, wanaendelea hadi leo hii katika kila kona ya dunia, kukumbuka kwa huzuni na majonzi jinai hiyo kubwa waliyofanyiwa watu wa nyumba tukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW na kumbukumbu hizo huwa kubwa zaidi katika siku kama ya leo ya mwezi kumi Muharram kila mwaka.

Waislamu katika nchi za Afrika kama vile Nigeria, Afrika Kusini, Ghana, Misri, Uganda, Tanzania, Kenya, Rwanda na Burundi wameandaa vikao na mijumuiko mbali mbali za maombolezo leo kwa mnasaba w Siku ya Ashura.

Dunia yakumbuka kuuawa Shahidi Imam Hussein AS na wafuasi wake 72 huko Karbala

3840766

captcha