IQNA

Khatibu wa Swala ya Ijumaa
17:26 - September 13, 2019
News ID: 3472128
TEHRAN (IQNA) - Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran ameashiria mapambano ya Kiislamu (muqawama) na kusimama kidete wananchi wa Syria, Lebanon, Iraq, Bahrain na Yemen mbele ya mabebebu na waistikabari na kusisitiza kuwa, somo la Ashura na harakati ya Imam Hussein AS ni chimbuko la muqawama wa wananchi wa eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).

Hujatul-Islam Wal-Muslimin Sayyid Muhammad Hassan Abu Turabi Fard amesema hayo leo mbele ya hadhara kubwa ya waumini waliohudhuria ibada ya Swala ya Ijumaa mjini Tehran  ambapo amebainisha kwamba, katika kipindi cha miaka Arobaini iliyopita, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamepata ushindi wa kukumbukwa kupitia mafundisho yatokanayo na mwamako wa Ashura.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran ameongeza kuwa, mafundisho ya mwamko wa Ashura hii leo yameibadilisha jamii ya mwanadamu na kuifanya kuwa jamii yenye utamaduni wa mapinduzi, kusimama kidete na kutosalimu amri mbele ya dhulma na ukandamizaji wa mabeberu.

Hujatul-Islam Wal-Muslimin Sayyid Muhammad Hassan Abu Turabi Fard amesema pia kuwa, Waislamu wanapaswa kumtambua adui na kueleza kwamba, Marekani na Waistikbari wa dunia wana wasiwasi mno na ushindi wa kambi ya muqawama na mapambano.

Kadhalika khatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo hapa mjini Tehran ameashiria vikawzo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kueleza wazi kwamba, kupata somo na funzo kupitia tukio la Ashura na harakati ya Imam Hussein AS kutapelekea kupata ushindi katika vita vya kiuchumi vya kila upande vya madola ya Magharibi.

Imam Husain AS aliuawa shahidi kikatili na kinyama mwaka wa 61 Hijria, yaani miaka 1380 iliyopita, katika jangwa la Karbala, Iraq ya leo, akiwa na umri wa miaka 57 baada ya kuongoza mapambano ya kishujaa ya ushindi wa damu mbele ya upanga. Imam Hussein AS aliuawa shahidi tarehe 10 Muharram na siku hiyo ni maarufu kama Siku ya Ashura.

Vita vya Karbala vilikuwa moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq. Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili ili kuilinda dini ya Allah. Hamasa ya Karbala ilikuwa dhihirisho la mambo mawili makuu. Kwanza ni ujasiri, ushujaa, moyo wa kujitolea, uaminifu pamoja na kuyapokea kwa moyo mkunjufu mauti ya kuuawa shahidi, sifa walizojipamba nazo wapiganaji wachache wa jeshi la haki wakiongozwa na Imam Hussein AS dhidi ya Yazid bin Muawiya. Pili ni upeo wa ukatili, udhalimu na unyama ulioonyeshwa na jeshi batili la Yazid bin Muawiya. Baada ya kupambana kishujaa, hatimaye mjukuu huyo wa Mtume Muhammad SAW aliuawa shahidi katika Siku ya Ashura.

3841790

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: