IQNA

19:21 - October 29, 2019
News ID: 3472193
TEHRAN (IQNA) – Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen ametahadharisha hujuma ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo na kusisitiza kuwa, amani haiwezi kurejeshwa nchini humo kupitia nguvu za kijeshi.

Abdul-Malik al-Houthi amesema hayo mjini Sana'a wakati alipokutana na kufanya mazungmzo  na Martin Griffiths, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen. Katika kikao hicho alibaini kuwa msimamo wa Saudia wa kushupalia uvamizi wa kijeshi umeshindwa kurejesha amani na usalama katika nchi hiyo ya Kiarabu na katika eneo la Asia Magharibi.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Ansarullah, Mohammed Abdul-Salam baada ya mazungumzo hayo ya Jumatatu  kati ya Al-Houthi na Griffiths imesema kuwa, wavamizi hao wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen.

Katika siku za karibuni, ndege za muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia zimeyashambulia mara kadhaa maeneo ya makazi ya raia katika mikoa ya Sa'dah na Hajjah.

Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha usukani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.

Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasio na hatia. Zaidi ya watu 16,000 wanaripotiwa kupoteza maisha katika vita vya Saudia dhidi ya Yemen. Idadi kubwa ya watoto na wanawake ni miongoni mwa waliopoteza maisha moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na vita dhidi ya Yemen vinavyoongozwa na Saudia kwa himaya ya madola ya Magharibi hasa Marekani na utawala haramu wa Israel.

3469757

 

Name:
Email:
* Comment: