IQNA

Rais wa Iran: Ulaya, Marekani hazitaki amani Yemen ili ziendelee kuuza silaha

19:21 - December 03, 2019
Habari ID: 3472254
TEHRAN (IQNA)- Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Ulaya na Marekani hazina azma ya kurejesha amani huko Yemen bali pande hizo zinafuatilia kuuza silaha zao.

Rais Rouhani amebaini kwamba kwamba nchi zote zinapaswa kufanya juhudi ili kuhitimisha haraka vita huko Yemen na kurejesha amani na uthabiti nchini humo chini ya kivuli cha mazungumzo ya amani kati ya makundi  ya Wayemen.

Akizungumza leo Jumanne hapa Tehran na Yusuf bin Alawi Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameutaja mgogoro wa Yemen kuwa moja ya kadhia na matatizo makubwa yanayolisibu eneo hili na kueleza kuwa vita vya Yemen havijawa na matunda yoyote ghairi ya kusababisha uharibifu, watu kuuawa, kuibua chuki baina ya watu wa nchi mbili na kutishia umoja wa adhi nzima ya Yemen.

Katika mazungumzo hayo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman hapa Tehran, Rais Rouhani ameashiria namna Iran isivyo na tatizo lolote la kustawisha uhusiano kati yake na jirani zake na kuangalia upya uhusiano kati yake na Saudi Arabia na kueleza kuwa: Siasa za serikali ya Saudi Arabia huko Syria, Iraq na Lebanon hazijawa na matunda kwa nchi hiyo na kwamba watawala wa nchi hiyo wanapasa kubadili mkondo wa siasa zao hizo.  

Rais wa Iran amesema kuwa nchi za eneo la Asia Magharibi zinapasa kushiriki katika kudhamini usalama wa eneo na kuwajibika ipasavyo katika uwanja huo. Amesema Iran imewasilisha Mpango wa Amani ya Hormoz kwa mtazamo huo.

Rouhani amesisitiza kuwa hakuna njia nyingine ghairi ya undugu na urafiki kati ya nchi na mataifa ya eneo  hili. Ameongeza kuwa hali ya usalama inapasa kudhaminiwa katika eneo hili khususan katika Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormoz na kutotoa mwanya kwa uingiliaji wa nchi ajinabi kupitia kuimarisha ushirikiano baina ya nchi za eneo.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Oman inaweza kuwa kituo kwa ajili ya biashara za Iran katika eneo na kusisitiza kuimarishwa ushirikiano kati ya nchi mbili hizi.

Katika mazungumzo hayo naye Yusuf bin Alawi Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman amekutaja kuimraishwa uhusiano na ushirikiano kati ya Iran na Oman kuwa ni kwa maslahi ya nchi zote za eneo hili na kuongeza kuwa: Ubunifu wa Iran katika kuwasilisha mpango wa Amani ya Hormoz bila shaka utakuwa kwa maslahi ya wote na kwa ajili ya kudumisha amani na usalama wa nchi za eneo. 

Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ikishirikiana na UAE zilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kutoroka nchi. Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasio na hatia wasiopungua 17,000 moja kwa moja katika vita hivyo. Makumi ya maelfu ya Wayemen pia wamepoteza maisha kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na vita hivyo. Idadi kubwa ya watoto na wanawake ni miongoni mwa waliopoteza maisha katika vita dhidi ya Yemen vinavyoongozwa na Saudia kwa himaya ya madola ya Magharibi hasa Marekani, Uingereza na utawala haramu wa Israel.

386148

captcha