IQNA

9:10 - January 08, 2020
News ID: 3472352
TEHRAN (IQNA) - Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limevurumisha makombora ya balestiki na kupiga kambi za kijeshi za Marekani nchini Iraq, kama jibu la kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha IRGC

Taarifa ya IRGC imesema kuwa, Iran imetoa jibu hilo kwa chokochoko za Marekani alfajiri ya leo, ambapo imelenga uwanja wa ndege wa kijeshi wa Marekani wa Ain al-Assad katika mkoa wa al-Anbar, magharibi mwa Iraq.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limeitaka Marekani iwaondoea wanajeshi wake wote katika nchi hiyo ya Kiarabu, likisisitiza kuwa halitatenganisha kati ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kujibu mapigo ya kuuawa shahidi Luteni Jenerali Soleimani.

IRGC imeonya kuwa, "Shetani mkubwa, yaani utawala wa kiistikbari wa Marekani utakabiliwa na vipigo vikali vya kuumiza, iwapo utachukua hatua nyingine ya kichokozi dhidi ya taifa kubwa la Iran." Taarifa ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu imeongeza kuwa, pigo hilo dhidi ya Wamarekani wavamizi ni ushindi mkubwa kwa umma wa Kiislamu ni taifa kubwa lisolotetereka la Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif ameashiria jibu hilo la Iran katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake wa Twitter na kuandika: "Iran imechukua hatua madhubuti ya kujihami kwa mujibu wa Sura ya 51 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kwa kulenga kambi ya jeshi ambayo ilitumiwa katika shambulizi la kioga dhidi ya raia na maafisa wetu wa ngazi za juu. Hatutaki kushadidisha hali ya mambo wala vita, lakini tutajihami dhidi ya uvamizi wowote."

Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imethibitisha habari hizo za kuvurumishwa makumi ya makombora ya balestiki kuelekea katika kambi ya kistratajia ya jeshi la Marekani nchini Iraq.

Mapema jana, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema kisasi cha taifa la Iran kwa damu ya kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Quds cha SEPAH kitakuwa kikali, madhubuti, cha kutisha na kamilifu.

3870124

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: