IQNA

Hamas yawataka viongoz wa nchi za Kiarabu, Kiislamu kusambaratisha mpango wa Israel

22:05 - June 10, 2020
Habari ID: 3472852
TEHRAN (IQNA) - Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) amewatumia barua tofauti wakuu na viongozi wa nchi za Kiarabu na Kiislamu zaidi ya 40 akiwataka kuchukua hatua za harakati kusitisha mpango wa Israel wa kutaka kuyaunganisha baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

 

Utawala wa Kizayuni umedhamiria kwa mujibu wa mpango wa Marekani na Wazayuni eti wa Muamala wa Karne na kwa kuungwa mkono na Rais Donald Trump wa Marekani kuunganisha asilimia 30 ya ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.   

Kitengo cha Upashaji Habari cha Palestina kimeripoti kuwa, Ismail Hania Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Hamas amesema katika barua hizo kwamba: Mpango wa kuunganisha sehemu ya ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni hatari ya wazi kwa hii leo na kwa mustakbali wa Palestina na kwa Umma wote wa Kiarabu na Kiislamu. 

Hania amewataka viongozi wa nchi za Kiarabu na Kiislamu kuitisha kikao katika ngazi ya viongozi cha kuunga mkono msimamo wa pamoja wa Wapalestina katika kupinga mpango huo wa kuyaunganisha maeneo ya UKingo wa Magharibi na Quds. 

Aidha ametaka kuandaliwa mkakati unaofaa wa kuunga mkono mpango wa kitaifa wa Wapalestina ili kurejeshewa haki zao za kisheria, kukombolewa ardhi zao na kuasisi nchi  huru ya Palestina ambayo mji mkuu wake utakuwa Quds.  

Aghalabu ya nchi, shakhsia, viongozi wa kisiasa na wale wa kidini katika pembe mbalimali duniani wamelaani vikali mpango huo wa kughusubu ardhi zaidi za Palestina katika eneo la Ukingo wa Magharibi. 

3904040

captcha