IQNA

Iran yaunga mkono kikao cha Umoja wa Mataifa kilichojadili ubaguzi wa rangi Marekani

13:24 - June 18, 2020
Habari ID: 3472875
TEHRAN (IQNA) – Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeunga mkono kikao maalumu cha Baraza la Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa ambacho kimeitishwa kujadili ubaguzi wa rangi nchini Marekani.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Sayyid Abbas Mousavi amesema Iran itatumia uwezo wake wote kusaidia Umoja wa Mataifa kukabiliana na tatizo la ubaguzi wa rangi. Amesema Iran ya Kiislamu daima imekuwa mstari wa mbele kukabiliana na ubaguzi wa rangi kwa kutegemea misingi ya kidini, kiutamaduni na kitaifa. Ameongeza kuwa, Iran ina azma ya kukabiliana na ubaguzi kote duniani hasa Marekani.

Kikao cha dharura cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kimefanyika Jumatano 17 Juni kwa lengo la kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu na ubaguzi wa rangi wa kimfumo nchini Marekani. Kikao hicho kimefanyika katika ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi.

Kikao hicho kimeitishwa kufuatia  baada ya kuuawa George Floyd, raia wa Marekani mweusi au mwenye asili ya Afrika katika mji wa Minneapolis.  Mnamo Mei 25, afisa mzungu wa polisi katika mji wa Minneapolis jimboni Minnesota nchini Marekani alimbinya shingo kwa kutumia goti kwa muda dakika 9 hivi Floyd, hadi akakata roho. Kikao hicho cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kimehudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa na kimeitishwa kufuatia ombi la nchi za Afrika. Akizungumza katika kikao hicho, Michelle Bachelet Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa amebainisha masikitiko yake makubwa kutokana na kuendelea ubaguzi wa rangi wa kimfumo nchini Markeani na hujuma za kinyama za polisi katika kukabiliana na wananchi wanaoandamana kwa amani nchini humo.

Amesema kuna udharura wa kuchukuliwa hatua za kivitendo kwa ajili ya kufanya marekebisho katika idara za polisi na mahakama nchini Marekani hasa ubaguzi wa rangi na utumiaji mabavu dhidi ya watu wa makundi ya waliowachache, watu wenye asili ya Afrika na Wamarekani asili.

Bachelet amesema mauaji ya George Floyds ni nembo ya ubaguzi wa rangi ulioratibiwa na kuongeza kuwa: "Hujuma za kibaguzi zinatokana na kushindwa kukabiliana na turathi ya zama za ukoloni na utumwa." 

Kikao hicho kilihutubiwa na Philonise Floyd ndugu yake George Floyd ambaye ametoa hotuba iliyojaa masikitiko  ambapo alibainisha namna ndugu yake alivyouawa kinyama mikononi mwa polisi. Ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuwasaidia Wamarekani weusi ambao wanakabiliwa na hujuma, ukatili na ubaguzi mikononi mwa jeshi la polisi na vikosi vya usalama Marekani.

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limetaka kufanyike mabadiliko katika hali ya hivi sasa nchini Marekani.

Tendayi Achiume, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ubaguzi wa rangi ametoa mifano kadhaa mauaji ya kinyama ya Wamarekani weusi mikononi mwa polisi na vikosi vya usalama Marekani. Ametaja ukatili huo dhidi ya watu weusi Marekani kuwa ni mgogoro na ametaka hatua imara zichukuliwe kukabiliana na hali hiyo.

83825248

captcha