IQNA

Wapalestina walaani mapatano ya kuaibisha ya UAE na Israel

11:02 - August 14, 2020
Habari ID: 3473065
TEHRAN (IQNA) - Wapalestina wanaendelea kulaani vikali hatua ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuanzisha rasmi uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ismail Haniyah, kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, amelaani vikali mapatano hayo yaliyofikiwa baina ya Marekani, utawala haramu wa Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu. Ameongeza kuwa,  Wapalestina wote wanaafikiana na Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kuhusu kuundwa nchi huru ya Palestina mji wake mkuu ukiwa ni Quds Tukufu (Jerusalem). Haniya amepinga vikali hatua yoyote ambayo inafuta haki za Wapalestina na inayokiuka maazimio ya kimataifa. 

Naye Fauzi Barhum, Msemaji wa Hamas ametoa taarifa kuhusu njama inayotekelezwa na Marekani iliyopelekea kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya UAE na utawala wa Kizayuni na Israel na kusema: "Mapatano baina ya UAE na Israel ni zawadi ambayo Abu Dhabi imepewa na utawala huo ghasibu wa Kizayuni kutokana na kuwasaliti Wapalestina."

Naye Dawud Shahab, mwanachama wa ngazi za juu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina amesema mapatano hayo ya UAE na Israel  yamefikiwa ili kumuokoa Benjamin Netanyahu ambaye anakabiliwa na mgogoro katika utawala wake.

Aidha amesema kuwepo uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni ni sawa na kujidhalilisha mbele ya adui na kusema mapatano yatampa adui Mzayuni kiburi cha kushadidisha uhasama dhidi ya Wapalestina.

Kwa upande wake  Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amelaani vikali mapatano hayo ya Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu na ametaka kufanyike kikao cha dharura cha viongozi wa Palestina kujadili mapatano hayo.

Mshauri wa ngazi za juu wa Mahmoud Abbas, Nabil Abu Rudeineh amesema mapatano hayo ya Israel na Imarati ni usaliti kwa Quds Tukufu (Jerusalem), Msikiti wa Al Aqsa na malengo matukufu ya kupigania ukombozi wa Palestina.

Siku ya Alhamisi, rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kufikiwa mapatano baina ya Umoja wa Falme za Kiarabu na utawala haramu wa Israel kuhusu kuanzishwa uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia baina ya pande mbili.

3472273

captcha