IQNA

Harakati ya Kenya-Palestina
16:16 - August 16, 2020
Habari ID: 3473073
TEHRAN (IQNA)- Harakati ya Mshikamano wa Kenya na Palestina imelaani vikali mapatano yaliyofikiwa baina ya watawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu na utawala ghasibu wa Israel chini ya usimamizi wa makundi ya Kizayuni nchini Marekani.

Katika taarifa, Kenne Mwikya, Katibu wa Harakati ya Mshikamano wa Kenya na Palestina amesema, baada ya miaka mingi ya uhusiano wa siri baina ya tawala za Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu, pande mbili hatimaye zimefikia mapatano ambayo yatapelekea kuanzishwa uhusiano wa chini ya usimamizi wa serikali ya Trump. Taarifa hiyo imesema mapatano hayo si kwa maslahi ya watu wa eneo bali ni kwa maslahi ya tawala hizo mbili. Harakati ya Mshikamano wa Kenya na Palestina imesema mapatano hayo yatatumika kuimarisha utawala wa Kizayuni ambao unakalia ardhi za Palestina kwa mabavu sambamba na kuwapa nguvu watawala wa Kiarabu ambao wanatekeleza jinai dhidi ya watu wa Yemen, Libya, Syria na Iraq.

Halikadhalika Harakati ya Mshikamano wa Kenya na Palestina imesema wakati ambao dunia ina wasi wasi kuhusu utawala wa Kizayuni kuendelea kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina na kuwanyima haki zao, msimamo uliochukuliwa na Umoja wa Falme za Kiarabu ni ukiukwaji mkubwa wa mshikamano wa kimataifa kwa ajili ya kuhitimisha ukaliwaji mabavu ardhi za Palestina na ukandamizaji wa taifa hilo unaotekelezwa na Israel.

Kenne Mwikya ameongeza kuwa Harakati ya Mshikamano wa Kenya na Palestina inajiunga na Wapalestina kuwalaani viongozi wa UAE ambao  wamewasaliti Wapalestina katika mapambano yao ya uhuru.

Aidha harakati hiyo imetangaza kuendelea kuunga mkono Wapalestina na imetoa wito kwa Umoja wa Afrika na jamii ya kimataifa kupinga muungano huo wa Israel na UAE kwa njia zozote zinazowezekana ili kuhitimisha masaibu ya muda mrefu ya Wapalestina. Halikadhalika Harakati ya Mashikamano wa Kenya na Palestina imetoa wito wa kususiwa Umoja wa Falme za Kiarabu hasa matamasha ya kiutamaduni, kicuhumi na kimichezo ambayo hufanyika katika nchi hiyo. Taarifa hiyo aidha imesisitiza kuhusu kususiwa safari zote katika ardhi zote za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zikiwemo zile ambazo zimepachikwa jina la ‘Israel’  na Msikiti wa Al Aqsa ulio katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu. 

472713

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* captcha: