IQNA

Watetezi wa Palestina

Rais wa Iran: Marekani na Israel zishtakiwe kwa mauaji ya kimbari Gaza

14:49 - December 24, 2023
Habari ID: 3478082
IQNA-Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria chimbuko la matukio ya hivi karibuni huko Palestina na kusema kuwa, Marekani na utawala wa Kizayuni zinapaswa kushtakiwa kwa kufanya mauaji ya kimbari huko Gaza.

Ayatullah Seyed Ebrahim Raisi alisema hayo alasiri ya jana katika Kongamano la Kimataifa la Kuunga Mkono Palestina ambapo amewashukuru wawakilishi wa nchi mbalimbali kwa uelewa wao na maafikiano kuhusiana na daghadagha na  hangaiko muhimu zaidi la ulimwengu wa Kiislamu hii leo bali ulimwengu wote wa ubinadamu na kueleza kwamba, hii leo mtazamo wa watu wote walio macho, wenye ufahamu na wenye dhamira safi duniani kote ni kwamba, wanalitazama suala la Palestina na ukiukwaji wa haki zote za binadamu huko Gaza kwamba, sababu yake ni mfumo kibeberu ambao haujali maadili, sheria na ubinadamu katika njia hiyo.

Sambamba na kusisitiza kuwa, mwenendo huu unapaswa kumfanya kila mtu afikirie, Rais Ebrahim Raisi amebainisha kwamba, mauaji makubwa ya wanawake na watoto na uharibifu wa makazi na nyumba za watu ni jambo la kusikitisha sana, lakini linaloumiza zaidi ni uungaji mkono usio na shaka wa nchi zinazodai kuwa watetezi wa haki za binadamu, kama vile Marekani na baadhi ya nchi za magharibi kwa jinai hizi.

Kadhalika Rais wa Iran ameeleza kuwa, linalotia simanzii zaidi ni kufeli asasi zote za kimataifa ambazo siku zote zimekuwa zikipiga ngoma ya usawa na uadilifu na kupinga dhulma.

Kongamano la Kimataifa la Kuunga Mkono Palestina lilifanyika jana hapa mjini Tehran kwa kuhudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu wa serikali, shakhsia mashuhuri wa kisiasa, kidini, kielimu na vyombo vya habari kutoka zaidi ya nchi 50 kwa lengo la kuunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi.

 

4189496

Habari zinazohusiana
captcha