IQNA

Wapalestina wailaani Bahrain kwa kuanzisha uhusiano na utawala bandia wa Israel

11:52 - September 12, 2020
Habari ID: 3473160
TEHRAN (IQNA)- Wapalestina wameulaani utawala wa Kifalme wa Bahrain kwa kuanzisha uhusiano na utawala bandia wa Israel.

Rais Donald Trump wa Marekani usiku wa kuamkia leo alitangaza kuwa Bahrain na Israel zimefikia mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina yao.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imelaani hatua hiyo na kusisitiza kuwa, uamuzi huo wa utawala wa Bahrain wa ukoo wa Aal Khalifa wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel ni jambo ambalo linanaupa nguvu utekelezaji wa vipengele vya mpango wa kihaini wa Muamala wa Karne ambao lengo lake ni kusambaratisha malengo matukufu ya Palestina.

Daud Shahab, mkuu wa masuala ya habari wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina, yeye mbali na kulaani hatua ya utawala wa Aal Khalifa ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni amebainisha kwamba, makubaliano hayo yanadhihirisha jinsi utawala wa Bahrain unavyoiabudu na kuitii Marekani.

Naye Hanan Ashrawi wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) amelaani vikali hatua hiyo ya Bahrain na kusema utawala wa Trump unatumia mbinuzi zote chafu za kisiasa na kiuchumi kuzishinikiza nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa kikoloni wa Israel.

Nchini Bahrain kwenyewe, harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo ya Al-Wifaq nayo pia imelaani hatua hiyo ya utawala wa Aal Khalifa na kusisitiza kuwa, wananchi wa Bahrain hawatayapuuza wala kuyasahau malengo matukufu ya Palestina.

Ikumbukwe kuwa utawala wa Bahrain umechukua hatua ya kusaliti malengo matukufu ya Palestina na Ulimwengu wa Kiislamu kwa kuamua kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, ukiwa umepita mwezi mmoja tu tangu Umoja wa Falme za Kiarabu nao pia kuchukua hatua kama hiyo ambayo imekosolewa vikali na kulaaniwa na  makundi ya Palestina, nchi za Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi na shakhsia kadhaa wa kisiasa, kijamii na kidini kote duniani.

Rais wa Marekani, Donald Trump amekuwa akifanya njama za kila namna za kuhakikisha nchi za Kiarabu zinakuwa na uhusiano wa kawaida na utawala pandikizi wa Israel. Siku ya Alkhamisi ya tarehe 13 Agosti, Umoja wa Falme za Kiarabu  na utawala wa Kizayuni zilifikia makubaliano ya kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia baina yao.

3472525

captcha