IQNA

Watunisia waandamana nje ya ubalozi wa UAE kupigana mapatano na Israel

22:30 - August 19, 2020
Habari ID: 3473085
TEHRAN (IQNA)- Wananchi wa Tunisia waliokuwa na hasira wameandamana nje ya ubalozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) mjini Tunis kupinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya UAE na utawala haramu wa Israel.

Kwa mujibu wa taarifa, maandamano hayo ya Jumanne yaliiitishwa na vyama vya kisiasa na makundi ya kiraia. Washiriki katika maandamano hayo wakiwa wamebeba bendera za Palestina na Tunisia pamoja na mabango ya kuunga mkono mapambano ya kupigiania ukombozi wa Palestina walisikika wakitoa nara za kupinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya utawala wa Kizayuni wa Israel na UAE.

Waandamanaji pia wameitaka serikali ya Tunisia ichukue hatua kali za kuzuia kuanzishwa uhusiano na utawala haramu wa Israel. Washiriki katika maandamano hayo wamependekeza kuwa, Bunge la Tunisia lipitishe sheria ya kuharamisha uhusiano na utawala wa Israel.

Kufuatia hatua kadhaa zilizochukuliwa na Rais Donald Trump wa Marekani kwa lengo la kurahisisha uanzishwaji wa uhusiano wa kawaida kati ya Imarati na utawala haramu wa Kizayuni, Alkhamisi iliyopita pande mbili za Abu Dhabi na Tel Aviv zilisaini mkataba na kuafikiana rasmi kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia.

Makubaliano hayo kati ya Israel na Imarati yamekabiliwa na wimbi kali la malalamiko na upinzani wa makundi ya Palestina, nchi za Kiislamu na shakhsia kadhaa wa kisiasa duniani, ambao karibu wote wamesisitiza kwa kauli moja kuwa, hatua hiyo ya Imarati ni uhaini na usaliti kwa malengo matukufu ya Palestina. 

3917611/

captcha