IQNA

Hamas: Marekani haijabadilisha sera zake kuhusu utawala wa Kizayuni

20:57 - September 30, 2021
Habari ID: 3474365
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) Ismail Haniya amesema rais Joe Biden wa Marekani na Naftali Bennet waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel hawaafiki utatutzi wowote wa kisiasa wa kadhia ya Palestina.

Katika mahojiano na televisheni ya Haber ya Uturuki, Haniya amesema Biden na Bennet hawaafiki hata suluhisho la kuundwa taifa la Palestina kwa msingi wa mipaka ya mwaka 1967.

Haniya ameongeza kuwa Biden na Bennet wanafuatilia zile zile sera za Israel kuendelea kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina. Amesema utawala wa sasa wa Israel unatekeleza sera za kupora ardhi zaidi na kukiuka haki za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Quds (Jerusalem) na Ukanda wa Ghaza.

Kuhusu mapatano eti ya amani baina ya Israel na baadhi ya tawala za Kiarabu, Haniya amesema Wapalestina wanasikitishwa na mapatano kama hayo huku akisema tawala hizo zinaamini kuwa uwepo wao unategemea uungaji mkono wa Marekani na kwamba njia ya kupata himaya ya Marekani ni kupitia Tel Aviv.

Kiongozi wa Hamas amesema mitazamoa ya wanachi wa nchi za Kiarabu inakinazana na maamuzi yaliyochukuliwa na watawala wa nchi hizo. Mwaka jana Morocco, Bahrain, Umoja wa Falme za Kiarabu zilianzisha uhusiano rasmi na utawala wa Kizayuni wa Israel na hivyo kujiunga na Misri na Jordan ambazo kwa muda mrefu zimekuwa  na uhusiano rasmi na utawala huo bandia.

3475849

captcha