Wabunge wa Ufaransa wamelaani kutekwa kwa meli hiyo ya misaada , wakisema ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa. Chama cha mrengo wa kushoto cha France Unbowed (LFI) kilisema katika taarifa kwamba kuwakamata wanaharakati waliokuwa kwenye meli hiyo ya misaada ni “ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.”
Utawala wa Kizayuni umeizingira Gaza tangu mwaka 2007, yaani kwa miaka 18, na unazuia misaada yoyote ya kibinadamu kutumwa kwenye ukanda huu. Baadhi ya wanaharakati wa haki za binadamu wanaopinga na kuhangaishwa na hali mbaya ya kibinadamu huko Gaza wanajaribu kupeleka misaada ya kibinadamu Gaza kwa kuzindua meli za uhuru (Freedom Flotilla) .
Katika harakati mpya ya kujaribu kuvunja mzingiro wa Gaza na kupeleka misaada kwa wakazi wa eneo hilo, meli ya urefu wa mita 18 ya Madleen ilianza safari yake Juni Mosi kutoka Bandari ya San Giovanni Li Cuti huko Catania, Sicily nchini Italia. Watu 12 wako ndani ya meli hiyo — wanaharakati 11 na mwandishi habari mmoja.
Miongoni mwao ni mwanaharakati wa mazingira kutoka Uswidi Greta Thunberg, Mbunge wa Bunge la Ulaya mwenye asili ya Kipalestina na Ufaransa Rima Hassan, Yasemin Acar kutoka Ujerumani, Baptiste Andre, Pascal Maurieras, Yanis Mhamdi na Reva Viard kutoka Ufaransa; Thiago Avila kutoka Brazil, Suayb Ordu kutoka Uturuki, Sergio Toribio kutoka Uhispania, Marco van Rennes kutoka Uholanzi na Omar Faiad, mwandishi wa Al Jazeera Mubasher kutoka Ufaransa.
Misaada ya dharura
Meli hiyo ilikuwa imesheheni misaada ya dharura inayohitajika kwa haraka na wakazi wa Gaza, ikiwa ni pamoja na maziwa ya watoto wachanga, unga, mchele, nepi, vifaa vya usafi kwa wanawake, vifaa vya kusafisha maji ya bahari, vifaa vya matibabu na vifaa vya watoto walemavu.
Wanajeshi wa utawala katili wa Israel waliwateka nyara wanaharakati waliokuwa ndani ya meli ya misaada ya kibinadamu ya Madleen iliyokuwa ikielekea Gaza, Jumapili usiku.
Kabla ya hapo Israel Katz, Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni alitangaza kuwa, jeshi la Israel lilipewa amri ya kutoiruhusu meli hiyo ya Madleen kufika Gaza.
Maana ya jina Madleen
Kuna sababu mbalimbali zilizoifanya Israel kuizuia meli hiyo kufika Gaza. Moja ya sababu za kwanza ni kwamba jina "Madleen" lilipewa meli hii kwa heshima ya "Madeleine Kollab", mvuvi wa kwanza wa kike wa Kipalestina huko Gaza; jina ambalo linaashiria uvumilivu na mapambano. Kwa hivyo, utawala wa Kizayuni una upinzani wa kisiasa na utambulisho na meli hiyo.
Ngao ya kibinadamu
Sababu nyingine muhimu ni kwamba, utawala wa Kizayuni unajaribu kuwatumia watu wa Gaza kama ngao ya kibinadamu dhidi ya Hamas kwa kuendeleza mzingiro na vita na kuzuia misaada ya kibinadamu isipelekwe Gaza. Tel Aviv inatumia sera ya kuwabakisha na njaa watu wa Gaza ili kuhamasisha maoni ya umma wa Gaza dhidi ya Hamas na kuishinda harakati hiyo ya Wapalestina kwa mbinu hii chafu na isiyo ya kibinadamu.
Kuwaadhibu watu wa Gaza
Sababu nyingine muhimu ni kuwa, utawala wa Kizayuni unawaadhibu watu wanaodhulumiwa wa Gaza kwa kuizuia meli ya Madleen na misaada ya kibinadamu kufika Gaza kwa sababu watu wa Gaza walikataa kuhamishiwa kwa lazima katika nchi nyingine na kung'ang'ania kubaki Gaza.
Kuhamishwa kwa lazima watu wa Gaza na kupelekwa katika nchi nyingine ulikuwa mpango wa utawala wa Trump nchini Marekani ambao ulikabiliwa na upinzani mkali wa watu wa Gaza kwa sababu ulimaanisha kukaliwa kwa mabavu Gaza kikamilifu na utawala wa Kizayuni.
Ujumbe wa kisiasa
Sababu nyingine ya mashambulizi ya wanajeshi wa Israel kwenye meli ya Madleen na kuizuia kufika Gaza ni kuzuia kufika ujumbe wa kisiasa wa meli hiyo.
"Zaher Birawi", mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Kuvunja Mzingiro wa Gaza, anaiona safari hii kuwa ni kilio cha upendo, amani na mshikamano; kulalamikia na kupinga ukimya wa serikali za dunia mbele ya mzingiro huo na kushindwa kuwapa mahitaji ya kimsingi Wapalestina zaidi ya milioni mbili.
Anasema: "Meli ni ndogo, lakini ujumbe wake ni mkubwa; ni nembo ya kukubali majukumu mataifa huru na mwito wa kukomesha jinai hii. Utawala wa Kizayuni hautaki ujumbe huu ufikishwe na meli ya Madleen.
Kwa ujumla inaweza kusemwa kuwa, mashambulizi ya wanajeshi wa Israel dhidi ya meli ya Madleen na kuzuia kufikishwa misaada ya kibinadamu huko Gaza ni ishara ya kushindwa jamii ya kimataifa kusimamisha jinai za utawala huo ghasibu.
3493394