IQNA

Televisheni ya Uganda yajadili kadhia ya umoja wa Waislamu

21:05 - November 23, 2020
Habari ID: 3473386
TEHRAN (IQNA) – Televisheni moja nchini Uganda imeandaa kipindi maalumu ambacho kimejadili vizingiti katika kufikia umoja baina ya Waislamu.

Kwa mujibu Shirika la Mahusiano ya Utamaduni wa Kiislamu (ICRO),  kitengo cha Kiislamu cha Televisheni ya Taifa ya Uganda (UBC) kimetayarisha kipindi hicho kwa ushirikiano na Kituo cha Utamaduni cha Iran nchini Uganda.

Mwambata wa Utamaduni wa Iran nchini Uganda Mohammadreza Qezelsofla na Rashid Kiwanuka, mkuu wa kitengo cha Kiislamu katika UBC pamoja na wawakilishi wa Ofisi ya Mufti wa Uganda na Baraza Kuu la Kiislamu Uganda walishiriki katika kipindi hicho.

Washiriki walijadili vizingiti katika njia ya Waislamu kufikia umoja na hali kadhalika haka ya ustawi na maendelo katika umma wa Kiislamu. Aidha walijadili umuhimu wa kuwafahamisha Waislamu kuhusu njama za maadui za kuvuruga umoja wao sambamba na haja ya kuzingatia mafundisho ya Qur’ani katika kadhia ya umoja. Halikadhalika walijadili miongozo ya Imam Khomeini MA na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu umoja.

Qezelsofla alisisitiza kuwa fikra za misimamo mikali ambazo zitaibua mifarakano miongoni mwa Waislamu zimekatazwa katika mafundisho ya Qur’ani Tukufu na Sirah ya Mtume Muhammad SAW.

Kwa upande wake, Rashid Kiwanuka amesema mafundisho ya Qur’ani Tukufu na Mtume Muhammad SAW hayana uhusiano wowote na misimamo mikali huku akisisitza kuwa, kuheshimiana, kuzingatia maadili ya Kiislamu, kusoma historia ya Kiislamu na kuwafahamu maadui wa Uislamu na njama zao ni nukta muhimu katika kuimarisha umoja wa Kiislamu.

3936854

captcha